Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jitihada za Kuvutia Watalii Ruvuma Hizi Hapa
Dec 20, 2023
Jitihada za Kuvutia Watalii Ruvuma Hizi Hapa
Picha ya watalii
Na Lilian Lundo - Ruvuma

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeanika jitihada inazozichukua ili kuvutia watalii mkoani Ruvuma.

Akizungumza leo mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ndg. Kanali Laban Thomas amezitaja jitihada hizo kuwa ni ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme wa REA ukarabati wa kiwanja cha ndege, maboresho kisiwani Lundo, na ununuzi wa boti ya watalii.

“Uhamasishaji umefanyika kupitia 'Royal Tour' na mpango Mkakati umeandaliwa ambapo maeneo ya vivutio yamefanyiwa maboresho kwa kupeleka wanyama katika kisiwa cha Lundo na kuletwa boti kwa ajili ya kuwapeleka watalii katika kisiwa cha Lundo na Mbambabay,” amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa.

Mkoa una vijiji 551 kati ya hivyo vijiji 480 sawa na asilimia 87.1 vimefikiwa na umeme katika Miradi ya REA na Vijiji 71 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya 3 Mzunguko wa pili kwa gharama ya shilingi Bilioni 99.6.

Vilevile mkoa huo, unatekeleza miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo, ujenzi wa barabara ya Mbinga Mbambabay kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 66 kwa kwa gharama ya shilingi bilioni 129.3, ujenzi wa barabara ya Amani Makoro - Ruanda (kilometa 35) kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 60.481.
 
Miradi mingine ni ukarabati na ujenzi wa Kiwanja Cha Ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.09 pamoja na ujenzi wa Bandari kubwa na ya kisasa ya Ndumbi katika ziwa Nyasa kwa gharama ya shilingi bilioni 12.2.

Ameendelea kusema, mkoa huo  ulikuwa na miradi ya maji 15, ambapo wananchi 120,000 walikuwa wanapata huduma ya maji safi na salama akisema kiwango cha upatikanaji maji mijini ilikuwa asilimia 50 na vijijini ilikuwa asilimia 57. Kwa sasa kuna jumla ya miradi 35 ya maji yenye jumla ya bilioni 51.2 inayoendelea  kuhudumia zaidi ya wananchi 264,000 na vijiji 81. Kiwango cha upatikanaji maji mijini imefikia asilimia 80.95 na vijijini imefikia asilimia 68.

Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiimarisha miundombinu, huduma za maji, na miundombinu ya usafiri katika maeneo yanayotembelewa watalii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi