Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jeshi la Polisi Lawashikilia Mgambo Waliompiga Raia Dar
Aug 31, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Fatma Salum-MAELEZO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kumshambulia na kumsababishia maumivu makali mtu anaetambulika kwa jina la Robson Orotho ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Bunju A Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Murilo Jumanne Murilo, imebainishwa kuwa sababu ya kushambuliwa kwa mfanyabiashara huyo ni kutokulipa faini ya usafi kiasi cha shilingi elfu 50.

Watuhumiwa hao watatu ni Kelvin Edson, Gudluck Festo na Rehema Nyange ambao wote ni Askari Mgambo wa Wilaya ya Kinondoni.

Aidha imeelezwa kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na taarifa mbalimbali zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilionesha kukiukwa kwa sheria za nchi, hivyo kupelekea Jeshi la Polisi kufanya ufuatiliaji wa haraka na kuwatia mbaroni watuhumiwa wote waliohusika na tukio hilo.  

Pia taarifa hiyo imesema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa vyombo vyote vya umma na visivyokuwa vya umma kufanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi