[caption id="attachment_39164" align="aligncenter" width="750"] Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihotubia Viongozi wa Majeshi na Serikali pamoja na Wananchi mbalimbali waliojitokeza katika hafla ya kufunga Mafunzo ambapo jumla Askari 513 wakiwemo Maafisa wa Polisi 120 na Wakaguzi Wasaidizi 393 wamehitimu katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini Jijini Dar es salaam.Desemba 21,2018[/caption]
Na.Immaculate Makilika – MAELEZO
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuwa na mwelekeo mpya wa kujenga uchumi wa kisasa, kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi wa viwanda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa viwanda na kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwatunuku vyeo wahitimu 513 waliofaulu zaidi mafunzo ya Uofisa na Ukaguzi, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es salaam, Rais Magufuli alisema kuwa imefika wakati Jeshi la Polisi kuwa na mwelekeo mpya wa uchumi wa kisasa ili kusaidia majeshi hayo kuwa na uwezo wa kujiendesha vizuri bila kutegemea sana Serikali.
“Mtafute mwelekeo mpya wa majeshi yetu, unaolenga kujenga uchumi wa kisasa, mjipange kushiriki shughuli za uchumi hasa ujenzi wa viwanda, pamoja na kupanua wigo wa kutengeneza sare zenu, na bidhaa mbalimbali za viatu au maji hali itakaosadia kuwa na bidhaa za ziada badala ya kununua na kuweza kujiendesha” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitolea mfano baadhi ya majeshi kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara ,ambapo alisema Jeshi la nchi ya China limejenga mji mkubwa nchini humo.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kushirikiana na majeshi mengine nchini likiwemo Jeshi la Polisi kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na kusaidiana masuala kadhaa.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameahidi kukipatia Chuo cha Taaluma ya Polisi nchini kiasi cha shilingi milioni 700 kabla ya ijumaa wiki ijayo kwa ajili ya kukarabati chuo hicho kwa kujenga mabweni na madarasa ya kisasa kwa lengo la kuboresha hali ya chuo na kuongeza ufanisi kwa wahitimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alisema ujenzi wa makazi ya Polisi unaendelea kwa kutumia fedha walizopewa na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 3.7, na wanatarajia kukarabati nyumba 400 za Polisi mara baada ya kupewa kiasi cha fedha kilichobaki ikiwa ni ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa mapema mwaka huu ya kuwapa Jeshi hilo shilingi bilioni 10 ambazo ameahidi kuwapa ndani ya kipindi cha wiki moja.
Vilevile, IGP Sirro, alisema kuwa nchi iko salama kwani hali ya uhalifu imepungua kwa kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kufanyakazi kwa kuzingatia nidhamu na weledi
“Hali ya uhalifu imepungua nchi nzima,makosa ya barabarani yamepungua kwa asilimia 32.6, ajali zimepungua kwa asilimia 30.8, kwa ujumla kumekuwepo na upungufu wa matukio ya uhalifu kwa sababu Jeshi la Polisi linashirikiana na wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao”alisema IGP Sirro
Naye, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Anthony Rutashugurugukwa, alisema kuwa mafunzo hayo yanayotolewa kwa lengo la kupanda daraja na vyeo yalidumu kwa muda wa miezi sita, ambapo wanafunzi 513 walihitimu masomo hayo yaliyogawanyika katika sehemu mbili za mafunzo ya Ukaguzi na Uofisa. Wahitimu wa mafunzo ya Uofisa walikuwa 120 ikiwa wanaume 106 na wanawake 14. Aidha, katika mafunzo ya Ukaguzi kulikuwa na wahitimu wanaume 393 na wahitimu wanawake 60.
Naibu Kamishna huyo wa Polisi alisema kuwa wahitimu hao wamepata mafunzo mbalimbali yakiwemo stadi za upelelezi, medani za kivita na masuala mengine mtambuka.