Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jaji Mkuu Atembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria.
Feb 02, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma na Maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye Maonesho ya Wiki ya utoaji wa Elimu ya Sheria na kutumia nafasi hiyo kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama.

 Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea maonesho hayo leo, Jaji Mkuu pia amewataka wananchi wenye malalamiko na maoni kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania kujitokeza na kutoa hizo ili ziweze kujibiwa na watumishi mbalimbali wa Mahakama walioko kwenye Maonesho hayo.

Jaji Mkuu pia ameto wito kwa wananchi wa Dodoma kufika na kuiuliza maswali Mahakama hasa juu ya ucheleweshwaji wa kesi zao na kuahidi kuwa maswali hayo yatajibiwa kwa lengo la hakikisha wanapata haki kwa wakati.

“Nawakaribisha wananchi wenye nafasi kufika kwenye viwanja vya Nyerere Square ili waweze kuona Mahakama ya Tanzania inavyofanya kazi zake kwa kushirikiana na wadau, ni wakati mzuri wa kutathmini utendaji wa Mahakama katika kipindi cha mwaka moja yaani tangu 2018” alisema Jaji Mkuu.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua hasa kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kesi.  Aliongeza kuwa kupitia Maonesho ya Wiki ya Sheria, wananchi watajifunza kuwasilisha kesi katika ngazi mbalimbali za Mahakama.

Akizungumzia mashauri kukaa kwa muda mrefu Mahakamani, Jaji Mkuu alisema Mahakama imekuwa ikilaumiwa kuchelewesha kesi lakini wakati mwingine kesi zimekuwa zikichelewa kwa kuwa ni lazima kesi ishughulikiwe na baadhi ya Taasisi wadau huku akitoa mfano kuwa kesi hupepelezwa na polisi lakini huendeshwa na Mwendesha Mashtaka.

Wiki ya Sheria imeanza jana Januari 31 jijini Dodoma na itamalizika Februari 5 ambapo siku ya Sheria nchini itaadhimishwa Februari 6, 2019 katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi