Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jafo Awataka Ma-DC Kuitumia Vizuri Sheria ya Kuweka Watu Ndani
Sep 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo - MAELEZO - Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewatakaa Wakuu wa Wilaya kuitumia vizuri sheria ya kumuweka mtu ndani kwa saa 48 pasipo uunevu wowote.

Jafo alitoa kauli hiyo jana Mjini Dodoma alipokuwa akifunga mafunzo ya Uongozi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Shinyanga na Dar es Salaam, Yalioanza Septemba 11, mwaka huu.

"Fanyeni kazi kwa kufuata mipaka yenu ya kazi, kwani ndilo jambo pekee litakalo waepusha na migogoro katika maeneo yenu ya kazi," alisema Jafo.

Aliendelea kwa kusema kuwa, viongozi hao wanapaswa kufanya kazi pasipo kumuone au kumpendelea mtu kwa namna yoyote ile, bali wakawe mifano kwa kujenga mahusiano mazuri na watumishi wanao waongoza pamoja na wananchi.

Kutokana na mafunzo waliyopata viongozi hao, Jafo amewataka kwenda kufanya mabadiliko katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, usimamizi wa miradi ya maendeleo, matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma.

Wakati wakiendelea na mafunzohayo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi aliwatembelea Wakuu hao wa Wilaya na kuwapa miongozo ya utendaji kazi pamoja na mipaka ya kazi yao ili kuepuka migogoro katika maeneo yao ya kazi.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo kutoka Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo alizitaja mada walizofundishwa viongozi hao kuwa ni pamoja na muundo wa Serikali, namna ya kumbadili kiongozi, utunzaji wa nyaraka na siri za Serikali, manunuzi, matumizi sahihi ya vyombo vya usalama, usalama wa nchi pamoja na mambo ya uchaguzi.

Taasisi ya Uongozi imekuwa ikiendesha mafunzo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa majijj, manispaa na halmashauri kwa awamu, ambapo mpaka sasa awamu nne zimeshafundishwa huku awamu ya mwisho ikitegemewa kufanyika Novemba mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi