Na Mwandishi wetu, Dar
Katika kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi, Serikali ya Italia imeahidi kuanzisha upya safari za ndege za moja kwa moja kutoka nchini humo hadi Zanzibar kuanzia tarehe 29 Juni, 2022.
Ahadi hiyo imetolewa na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Natalia amesema kuwa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar zitasaidia kukuza biashara na utalii baada ya kusitishwa kwa safari hizo tangu mwaka 2019 kutokana na changamoto ya Uviko 19.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuanzishwa upya kwa safari hizo kutachangia kukuza pato la taifa kwani awali kabla ya janga la Uviko 19, Zanzibar ilikuwa inapata watalii 200,000 kwa mwezi kutoka nchini Italia.
“Safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia kuja Zanzibar zinategemea kuanza rasmi tarehe 29 Juni, 2022 na tunaamini kuwa kuanzishwa kwa safari hiyo kutachangia kukuza sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Balozi Mbarouk
Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, utalii, viwanda, maji, kilimo, nishati, pamoja na maendeleo ya sekta binafsi.