Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

ILO Yaahidi Kushirikiana na Serikali Kuimarisha Usalama na Afya Kazini
Apr 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Sarah Reuben na Ahmed Sagaff - DODOMA

Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kuongeza ufanisi wa kushughulikia fidia kwa wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.

Ahadi hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mwakilishi wa shirika hilo, Ndg. Getrude Sima alipotembelea banda la mfuko huo katika maonesho yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano Jakaya Kikwete ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi inayoadhimishwa Aprili 28 kila mwaka.

“Tutaendelea kushirikiana na WCF kupitia mikakati yetu mbalimbali ndani ya Shirika la Kazi duniani hapa Tanzania kwa hiyo niwapongeze sana na nimefurahi kuona kwamba nanyi pia mmeweza kushiriki na kuwaeleza wananchi mnachofanya,” ameeleza Ndg. Sima.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini katika mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar amesema WCF imewahudumia watu mbalimbali waliopata ajali wakiwa kazini.

“Pamoja na huduma tunazozitoa, tunashirikiana na OSHA katika kuzuia ajali mahala pa kazi, pia tunashirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia ajali za barabarani,” amehabarisha Dkt. Omar.  

Sambamba na hayo, mnufaika wa mfuko huo, Ndg. Deus Anthony ameishukuru Serikali kwa kumtibu, kumnunulia mguu wa bandia na kumlipa pensheni kila mwezi ambayo ataendelea kupokea mpaka mwisho wa uhai wake.

“Mbali na pensheni ninayopata, nimejiajiri kwa kufanya kazi ya udereva wa bajaji, nashukuru sana kwani naihudumia familia yangu kama nilivyokuwa kabla ya ajali,” amearifu Anthony.

Naye Ndg. Hamisi Omari ameshukuru kwa kutibiwa, kununuliwa mkono wa bandia na kulipwa pensheni kila mwezi.

Naye Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda ameipongeza WCF kwa kupata tuzo mbalimbali.

WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha tano cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wanaumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi