Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

IAA Yaanzisha Kozi za Uanagenzi Kuwaandaa Vijana kwa Soko la Ajira
Feb 20, 2026
IAA Yaanzisha Kozi za Uanagenzi Kuwaandaa Vijana kwa Soko la Ajira
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, Akizungumza na Waandishi wa Habari Kuhusu Miradi ya Maendeleo na Fursa kwa Vijana, katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma.
Na Baraka Messa – MAELEZO

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeanzisha mfumo wa utoaji mafunzo kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship) ili kuwaandaa vijana kukabiliana na ushindani wa soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.

Mkuu wa chuo hicho, Prof. Eliamani Sedoyeka akizungumza na vyombo vya habari Februari 20, 2026 jijini Dodoma amesema hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya kimkakati ya chuo kuhakikisha wahitimu wanapata maarifa ya darasani sambamba na uzoefu wa kazi kwa vitendo.

Amesema kati ya kozi 27 za Shahada ya Kwanza zinazotolewa na IAA, kozi tatu tayari zinatolewa kwa mfumo wa Uanagenzi kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi na taasisi mbalimbali katika sekta za benki, bima na utalii.

Kozi hizo ni Shahada ya Usimamizi wa Utalii na Ukarimu na Uanagenzi (Bachelor of Tourism and Hospitality Management with Apprenticeship), Shahada ya Usimamizi wa Bima na Uanagenzi (Bachelor of Insurance and Risk Management with Apprenticeship) pamoja na Shahada ya Benki na Uanagenzi (Bachelor of Banking with Apprenticeship).

“Kupitia mfumo huu, mwanafunzi anasoma darasani lakini wakati huo huo anakuwa sehemu ya mazingira halisi ya kazi. Hii inamjengea uzoefu, nidhamu ya kazi na uelewa wa mahitaji ya waajiri,” amesema Prof. Sedoyeka.

Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya masomo, wanafunzi hugawanya muda wao sawa kati ya darasani na eneo la kazi, hali inayowawezesha kuhitimu wakiwa tayari wameiva kitaaluma na kiutendaji.

Kwa mujibu wa Prof. Sedoyeka, mfumo huo umeanza kuonyesha matokeo chanya kwa kuwa wahitimu wanakuwa na nafasi kubwa ya kuajiriwa mara tu wanapomaliza masomo yao, huku wengine wakianzisha shughuli zao binafsi kutokana na ujuzi na uzoefu walioupata.

Ameongeza kuwa IAA, ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha, inatoa mafunzo kuanzia ngazi ya astashahada (certificate) hadi shahada ya uzamili (Master’s Degree) katika fani mbalimbali zikiwemo uhasibu, fedha, uchumi, kodi, benki, bima, utalii, usimamizi wa biashara, TEHAMA, usimamizi wa rasilimali watu, mawasiliano ya umma, ununuzi na ugavi, uwekezaji, usimamizi wa miradi pamoja na usalama wa mtandao.

Chuo cha Serikali cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeanzisha mfumo wa utoaji mafunzo kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship) ili kuwaandaa vijana kukabiliana na ushindani wa soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.

Chuo cha Serikali cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeanzisha mfumo wa utoaji mafunzo kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship) ili kuwaandaa vijana kukabiliana na ushindani wa soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi