Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

IAA Kuwa Kinara wa Mapinduzi Ya Kidijitali Nchini
Feb 20, 2026
IAA Kuwa Kinara wa Mapinduzi Ya Kidijitali Nchini
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, Akizungumza na Waandishi wa Habari Kuhusu Miradi ya Maendeleo na Fursa kwa Vijana, katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma.
Na Naishooki Makeseni – MAELEZO

Serikali kupitia Chuo cha Uhasibu Arusha inaendelea kuchukua hatua za kimkakati kuimarisha mageuzi ya kidijitali katika elimu ya juu, ambapo kupitia chuo hicho imeanza  rasmi ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Data kitakachokuwa nguzo ya uhuru wa kidijitali nchini.

Akizungumza leo Februari 20, 2026 katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya kimkakati yanayolenga kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha maarifa na ubunifu wa kidijitali.

“Katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maarifa na ubunifu wa kidijitali, IAA imezindua mageuzi makubwa yatakayoongeza uhuru wa kidijitali, ubora wa elimu na ushindani wa kitaifa,” amesema Prof. Sedoyeka.

Amesema uwekezaji huo unatekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ukiweka msingi imara wa mustakabali wa elimu ya juu unaotegemea teknolojia na usalama wa taarifa.

Amesema kituo hicho  kitapunguza utegemezi wa upangishaji wa nje, kuimarisha usalama wa mtandao, na kuhakikisha mifumo ya kitaaluma na kiutawala inapatikana muda wote bila hitilafu.

Pia amesema kitasaidia kuhifadhi data za tafiti ndani ya mipaka ya nchi, kuongeza uaminifu wa mifumo ya kidijitali na kuimarisha ulinzi wa taarifa muhimu za taasisi na taifa kwa ujumla.

Prof. Sedoyeka amesisitiza kuwa uwekezaji huo wa kimkakati unaiweka IAA katika nafasi ya kinara wa mapinduzi ya kidigiti katika sekta ya elimu ya juu nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi