Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Huduma za Posta Afrika Zipo Katika Nafasi Nzuri Kuleta Ufanisi - Kakele
Jan 19, 2024
Huduma za Posta Afrika Zipo Katika Nafasi Nzuri Kuleta Ufanisi - Kakele
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Celestine Kakele akizungumza jana tarehe 18 Januari, 2024 wakati wa Maadhimisho ya 44 ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) yaliyofanyika jijini Arusha katika jengo la Makao Makuu ya Umoja huo (PAPU Tower),
Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Celestine Kakele amesema huduma za posta barani Afrika ziko katika nafasi nzuri ya kuleta ufanisi mzuri, faida na huduma nzuri za  kibiashara kwa jumuiya ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

Ameyasema hayo jana tarehe 18 Januari, 2024 wakati wa Maadhimisho ya 44 ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) yaliyofanyika jijini Arusha katika jengo la Makao Makuu ya Umoja huo (PAPU Tower),

“Kwa kuwa tayari tuna  mfumo wa NAPA, Tanzania imeweka msingi imara wa uendeshaji wa huduma za posta nchini na umeendana na matazamio ya wateja wake na utakuwa mwarobaini wa kuimarisha huduma za posta,” amesema.

Kwa upnde wake Posta Masta Mkuu, Maharage Chande amesema shirika hilo limejizatiti vyema katika kuimarisha huduma za posta nchini na Afrika kwa ujumla na kwamba wametambua uendeshaji wa huduma za posta umebadilika na unaendana zaidi na teknolojia mpya ambapo hata vijana hawatumii tena barua kama hapo zamani.

“Kwa kifupi tunakuja na mabadiliko makubwa kabisa na vitu ambavyo mtaanza kuviona kutoka posta, tutaanza kutumia teknolojia ili kuleta tija kwa wananchi na tutaanza kutumia zaidi ‘e-commerce’ kupitia duka mtandao na kurudisha huduma ya ‘money order’,” amesema.

Aidha Waziri wa TEHAMA na Posta wa Zimbabwe, Mhe. Tatenda Annastacia amesema ni muhimu na lazima huduma za posta ziwe za kidijitali ili zifanyike kwa ufanisi.

“Ni lazima sisi kama mawaziri lazima tukae pamoja na tulisimamie ili suala la uboreshaji wa huduma hizi ili ziwe za kidijiti kutokana na mwelekeo wa dunia ya sasa katika kurahisisha na kuharakisha mawasiliano na huduma za posta. Kikubwa ni lazima tuje na mwongozo ambao utatuongoza wote ili twende njia moja,” amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Dkt. Sifundo Chief Moyo amesema katika kuadhimisha miaka 44 ya Umoja wa Posta Afrika ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha kujengwa kwa Umoja wa Posta Afrika jijini Arusha.

“PAPU inatoa kila aina ya shukurani kwa kujengwa kwa makao makuu yake katika ardhi ya Tanzania na pia tuko tayari kushirikiana na Shirika la Posta na TCRA pia katika kuboresha huduma za posta hapa nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi