Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Historia Yaandikwa; JNHPP Yaingiza Megawati 235 Gridi ya Taifa
Feb 26, 2024
Historia Yaandikwa; JNHPP Yaingiza Megawati 235 Gridi ya Taifa
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitangaza kuhusu mradi wa Julius Nyerere kuingiza megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa katika eneo la mradi, Rufiji mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati 2,115 umeanza kazi na kuingiza  megawati 235 katika Gridi ya Taifa kupitia mtambo Namba 9.

 

Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kuwa mtambo huo ungeanza kuzalisha umeme tarehe 25 Februari 2024, ahadi iliyotimizwa siku tatu kabla kuanzia tarehe 22 Februari 2024 mtambo huo ulipoanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 25 Februari 2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa baadhi ya Wakuu wa Vyombo vya Habari na Wahariri katika eneo la mradi wilayani Rufiji mkoani Pwani ambapo Wahariri hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Bwawa la kuhifadhi maji yatakayozalisha umeme, tuta kuu na mitambo ya umeme.

Ameeleza kuwa, kuingia kwa megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa kumeboresha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza upungufu wa umeme kwa zaidi ya asilimia 85.

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitazama ujazo wa maji katika bwawa kwenye mradi wa Julius Nyerere ambao umeanza kuingiza megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa.

 

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere unaendelea na ifikapo mwezi Machi 2024 megawati nyingine 235 zitaingia katika gridi kupitia mtambo namba 8 na kufanya JNHPP kuingiza megawati 470 kwenye gridi na hivyo kupelekea nchi kuwa na ziada ya umeme ya megawati 70.

 

Amesema utekelezaji wa mradi huo ni jitihada za Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuta mradi huo ukiwa na asilimia 33 na sasa mradi huo unafikia mwisho.

 

Amesema, Dkt. Samia anaijali nchi kwa dhati na sasa mipango yake ya maendeleo haiangalii kipindi cha sasa tu bali miaka 30 hadi 40 ijayo na ndiyo maana ameshaagiza uendelezaji wa vyanzo vipya vya umeme ikiwemo gesi, maji na nishati jadidifu inayojumuisha jua, upepo na jotoardhi.

Dkt. Biteko pia amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kutekeleza mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018.

 

Muonekano wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115

 

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, utekelezaji wa JNHPP hauifanyi Wizara ya Nishati na Taasisi zake kubweteka na kutegemea umeme kutoka mradi huo pekee bali kasi ya utekelezaji wa miradi mingine mipya inaendelea ikiwemo mradi wa Rumakali (222MW), Ruhudji  (358) na miradi ya Jotoardhi ya Ngozi na Kiejo-Mbaka pamoja na mradi wa umeme Jua wa Kishapu (150MW).

 

Kuhusu utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa

mazingira ambao ndio unasababisha mabwawa ya umeme kuwa na maji ya kutosheleza kuzalisha umeme na pia kutoa elimu kuhusu athari za kuharibu vyanzo vya maji vinavyopeleka maji pia katika mabwawa ya umeme.

 

Kwa wananchi wanaozunguka maeneo yenye mitambo ya kuzalisha umeme, Dkt. Biteko amesisitiza TANESCO ihakikishe hawapati changamoto ya umeme kwani hao ndio walinzi wa maeneo hayo na mradi unapofika katika eneo lolote lazima ubadilishe hali ya wananchi katika eneo husika kwa namna mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii.

 

Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO na kampuni ya usimamizi wa mradi ya TECU kwa utekelezaji na usimamizi madhubuti wa mradi ambao umewezesha kuingiza megawati 235 kwenye gridi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa, ujazo wa maji unaohitajika katika bwawa la umeme la JNHPP ni mita za ujazo bilioni 32.7 na sasa kuna mita za ujazo bilioni 28 hivyo bado mita nne tu bwawa hilo kujaa kabisa.

 

Amesema kuwa, makadirio ni kuwa mita nne zilizobaki zitajaa mwezi huu kupitia usimamizi madhubuti wa Bonde la Maji la Rufiji.

 

Ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutofanya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji pia wasichepushe maji kiholela.

 

 

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, mradi huo ni muhimu katika kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Pwani kuwa mkoa wa kimkakati kwa kujenga viwanda vingi zaidi ambavyo kufanya kwake kazi kunategemea nishati ya umeme ya uhakika.

 

 

 

Amesema kuwa, mahitaji ya umeme mkoani Pwani ni megawati 130 lakini bado hayatoshelezi mahitaji hivyo mradi wa JNHPP kupitia kituo cha umeme cha Chalinze kitawezesha mkoa huo kupata umeme wa uhakika ambao utachochea wawekezaji wapya.

 

 

 

Ameongeza kuwa, kwa sasa Mkoa wa Pwani una viwanda 1,533 ambapo katika Serikali ya Awamu ya Sita viwanda 30 vinajengwa huku 17 vikiwa ukingoni kumalizika, hivyo mradi wa JNHPP ni muhimu katika kufanya viwanda hivyo kufanya uzalishaji.

 

Meneja Mradi kutoka kampuni zinazotekeleza mradi huo (Arab Contractors na Elsewedy Electric) Mohamed Zaky, amesema kuwa kampuni hiyo inaona fahari kufikia hatua hiyo ya uzalishaji na kwamba nia yao ni kutimiza ndoto ya Tanzania kuzalisha megawati 2,115 kupitia mradi wa JNHPP.

 

 

 

Aidha, amempongeza Dkt. Doto Biteko kwa msukumo anaoutoa kwa wakandarasi hao ili kutekeleza mradi kwa wakati na pia kwa kuusimamia kwa karibu mradi husika.

 

 

 

Viongozi wengine walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Mteule Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi