Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

HESLB Yatoa Tuzo kwa Waajiri Bora Sekta Binafsi Dodoma
Jun 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eline Maronga,HESLB,

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) imewatambua na kuwapa tuzo maalum waajiri 10 kutoka Mkoa wa Dodoma kutokana na kuwasilisha kwa wakati makato ya wafanyakazi wao waliokopeshwa.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi ngao iliyofanyika Juni 10, 2022 Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, amesema waajiri hao wamekuwa mfano kwani wamekuwa wakikata kwa wakati fedha za wafanyakazi wao kiasi cha asilimia 15 katika mshahara na kuwasilisha HESLB kupitia Mfumo wa Ki-elektroniki wa Malipo ya Serikali (GePG). 

“Tumeamua kuwatambua waajiri hawa kutoka sekta binafsi ili kuwahamasisha waajiri wengine ambao utekelezaji wao wa masharti ya Sheria ya HESLB sio mzuri kama inavyotarajiwa,” amesema Badru katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma na kuongeza:

“Kwa Mkoa wa Dodoma pekee, tunakusanya wastani wa TZS 5.7 bilioni kwa mwaka kutoka sekta binafsi ambayo ni sawa na asilimia 7.5 ya jumla ya TZS 76 bilioni tunazokusanya kwa mwaka kutoka sekta binafsi nchini kote hivyo tunashukuru sana kwa kutuunga mkono,” amesema Badru na kufafanua kuwa wataendelea kuwatambua waajiri katika mikoa mingine.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa HESLB Ofisi ya Dodoma, Octavia Seleman amewataja waajiri hao bora zaidi kwa Mkoa wa Arusha ni Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT); Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Peter Claver; Shule ya Sekondari Maria De Mattias; Shule ya Msingi Santhome; na Shule ya Martin Luther. 

Waajiri wengine ni Shirika la Health Promotion and Systems Strengthening (HPSS); Shirika la Helvetas Swiss Interco-operation; Taasisi ya Tanzania Research and Career Development; na Shirika la Inades-Formation Tanzania.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa urejeshaji mikopo kutoka sekta binafsi kwa Kanda ya Dodoma inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida na Tabora, Meneja Octavia amesema katika miaka sita iliyopita kiwango cha makusanyo kwa mwaka kimeongezeka kutoka TZS 1.2 bilioni mwaka 2016/2017 hadi TZS 5.7 bilioni mwaka 2021/2022.

“Mwaka 2017/2018 tulikusanya TZS 3.3 bilioni; mwaka 2018/2019 TZS 4.6 bilioni; mwaka 2019/2020 TZS 5.4 bilioni; mwaka 2020/2021 TZS 4.3 bilioni na mwaka 2021/2022 ni TZS 5.7 bilioni … hivyo kuna ongezeko kubwa na tunawashukuru sana,” amesema Octavia Seleman.

Akizungumza katika hafla hiyo wa niaba ya waajiri, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT), Godlisten Moshi ameishukuru HESLB kwa kuwatambua waajiri hatua ambayo inawatia moyo.

“Sisi CCT tunahudumia masikini, tunapoona kuna wadau wanahangaika kukusanya fedha ili kusomesha wasio na uwezo, tunajua hatupo peke yetu na tunaipongeza Serikali kupitia HESLB kwa kazi kubwa mnayofanya, tunaahidi kuunga mkono,” amesema Moshi ambaye taasisi yake nayo ilipata tuzo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi