Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Halmashauri Zatakiwa Kutumia Fedha za Mgawo wa Ada ya Wanyamapori  Kutoa Ulinzi kwa Wananchi
May 16, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo 

Serikali  imezitaka Halmashauri za Wilaya Nchini zinazopata mgawo wa mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.

Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Leah Jeremiah Komanya juu ya lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake.

"Takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu  vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali," alisema Mhe. Hasunga.

Aidha amesema, Wizara imekuwa ikitoa mgawo wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya wilaya husika.

Hata hivyo amesema, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukalisha mfumo wa kielektroniki  ujulikanao kama "MNRT Portal" ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo .

Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 01 Julai, 2018 ambapo nakala ngumu za taarifa zitakuwa zikitumwa kwenda wilaya husika.

Wakati huo huo Mhe. Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Salum Msabaha juu ya mkakati wa Serikali katika kuboresha vivutio vya utalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi na kukuza pato la Taifa, amesema Wizara imeandaa mkakati wa kuvitambua na kuvitangaza vivutio vyote nchini ukiwemo mji wa Bagamoyo.

Amesema mpango unalenga kushirikisha mashirika yaliyo chini ya Wizara yaani Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAMWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Ameendelea kusema,  vituo vya malikale vilivyopo Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo yatakayoendelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika hayo. Aidha, vivutio vyote vya utalii nchini vitaendelea kutangazwa kupitia Taasisi zinazohusika ikiwemo Bodi ya utalii Tanzania (TTB).

Ametaja kazi zitakazotekelezwa na mashirika hayo kuwa ni kuweka huduma muhimu kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususani majengo na barabara ili kuwezesha kufikika kwa urahisi na kuwa na muonekano unaovutia , kujenga vituo vya kumbukumbu na taarifa pale ambapo vinahitajika, kuboresha vioneshwa na kuvitangaza , kuhamasisha wawekezaji wa hoteli, michezo na vivutio vingine vya watalii.

Hata hivyo, Wizara ya MaliAsili na Utalii itaendelea kusimamia majukumu yote ya uhifadhi, utafiti na kuandaa taarifazitakazosaidia kuboresha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kwa kutoa elimu kwa Umma juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale na maliasili za nchi yetu.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi