Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Halmashauri Zatakiwa Kutenga Maeneo ya Kilimo kwa Vijana
Aug 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_34148" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Mh. Anthony Mavunde, akisisitiza jambo kuhusu siku ya kimataifa ya vijana duniani ambayo itaadhimishwa kitaifa mkoani Arusha tarehe 12 Agosti, 2018. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “MAZINGIRA SALAMA KWA VIJANA”. (Picha na: Abuu Kimario)[/caption]

Na. Georgina Misama - MAELEZO

Halmashauri zote nchini zimetakiwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya Vijana kuyatumia katika shughuli za kilimo.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira  Mhe. Antony Mavunde wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maadhisho ya siku ya Vijana Duniani.

Mavunde alisema hadi hivi sasa Serikali imetenga takribani hekta laki mbili katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwapa vijana fursa ya kuyatumia katika shughuli za kilimo.

"Nazitaka Halmashauri zote nchini ambazo bado hazijatenga maeneo hayo, kufanya hivyo ili kuendana na kauli mbiu ya mwaka 2018 inayosema 'Mazingira salama kwa Vijana' ambapo serikali ina wajibu wa kuandaa mazingira hayo kwa vijana." alisema Mavunde.

Akiongelea kuhusu mwitikio wa vijana kwenye shughuli za kilimo, Mavunde alisema kuwa vijana wengi wameanza kujishughulisha katika kilimo na ipo mifano mingi hai ya vijana walioamua kujiajiri kwenye kilimo biashara kama SUGEKO na wanafanya vizuri.

Wakati huo huo Mhe. Mavunde amesema kuwa,  Agosti 11 litafanyika kongamano kubwa la Vijana na Wadau wa Maendeleo ya Vijana katika Ukumbi Wa Mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo.

kilele cha Maadhimisho hayo ni Agosti 12 Mwaka huu, ambapo Mhe. Antony Mavunde (Mb) anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika tamasha la vijana ambalo litafanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu wa Elimu Maalum Patandi kilichopo Tengeru  litakalowashirikisha wadau mbalimbali wa Maendeleo ya vijana.

"Natoa wito kwa vijana wote nchini, wazazi na wadau wa Vijana washerehekee siku hii muhimu ili kwa pamoja tuonyeshe na kutambua umuhimu wa vijana kama washiriki wa Maendeleo ya nchi yetu, aidha nawaomba Vijana wote Tanzania wajitokeze na kushiriki katika Maadhimisho haya" alisema Mavunde.

Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni "Mazingira Salama kwa Vijana"

Mwaka 1999 Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha azimio Na. 54/120 la kuifanya tarehe 12 Agosti ya kila mwaka kuwa siku ya Vijana Duniani.Tanzania ilianza kuadhimisha siku hiyo mwaka 2000, ikiwa ni pamoja na nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa.

           

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi