Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hali ya Usalama Nchini ni Shwari – IGP Sirro
May 31, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_2185" align="aligncenter" width="730"] Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania – IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam leo.[/caption]

Na Eliphace Marwa.

Jeshi la Polisi limewahakikishia watanzania kuwa hali ya usalama nchini iko vizuri pamoja na kuwepo na matukio machache ya uhalifu katika baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakijitokeza.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.

Sirro amesema kuwa pamoja na nchi kuwa shwari, yapo matukio ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja, alitaja matukio hayo kuwa ni pamoja na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia katika Mkoa wa Pwani, Bodaboda kutokutii Sheria za usalama barabarani na kujihusisha na vitendo vya uhalifu na rushwa.

[caption id="attachment_2186" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania – IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam leo.Kushoto ni Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa.[/caption]

“Matukio yanayoendelea hivi sasa ni suala la muda tu, sasa tunakwenda kuyamaliza niseme tu hata hiki kikundi kinachofanya uhalifu katika maeneo ya Ikwiriri, Mkuranga na Kibiti hawajatuzidi nguvu, wao wako wachache, sisi tuko wengi, wafikishieni salamu zao,” alisema Kamanda Sirro.

Akizungumzia mauaji hayo ya Mkoani Pwani, IGP Sirro amesema kuwa kufuatia matukio hayo Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni mbalimbali za kuhakikisha vitendo hivyo haviendelei, sambamba na kuwasaka wahusika wote ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao wapo baadhi ya wahusika wamekwisha tiwa mikononi mwa Jeshi hilo.

[caption id="attachment_2191" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania – IGP Simon Sirro akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari kwa lengo la kuelezea mikakati yake ofisini kwake Jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kulia ni Kamshna wa Elice Mapunda na Kamishna wa Intelijensia ya Jinai Robert Boaz na Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa.(Picha na Frank Shija).[/caption]

Aidha Kamanda Sirro ameonya tabia ya wananchi kujichukulia Sheria mikononi kwa kuwapiga,kuwachoma moto, kuwaua na kuwadhalilisha kwa kuwavua nguo baadhi ya wananchi wanaoshukiwa kuwa ni wahalifu.

“Takwimu zetu zinaonyesha kuwa tabia hii ya kujichukulia Sheria mikononi inazidi kukua ambapo matukio 245 yameripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Machi ukilinganisha na matukio 222 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho Mwaka 2016,” alifafanua Kamanda Sirro.

Katika hatua nyingine Kamanda Sirro amewataka madereva wa bodaboda kuacha tabia ya kukaidi kufuata Sheria za usalama barabarani ikiwemo kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu pamoja na kutokuvaa kofia ngumu.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania –IGP Simon Sirro amekutana na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu kuanza kazi rasmi baada ya kuteuliwa na kuapishwa kushika wadhifa huo ambao awali ulikuwa ukishikiliwa na Ernest Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi