Na Paschal Dotto-MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa hakuna mwananchi anayeondolewa Loliondo bali Serikali inawaongezea Wananchi ardhi kwa matumizi yao.
Akizungumza katika Mkutano wa Wizara hiyo na Mabalozi Wanaowakilisha nchi zao, Balozi Mulamula alisema kuwa Serikali imeongeza eneo la matumizi ya ardhi kwa wananchi wa Loliondo kwa kuweka mipaka lakini wananchi wa eneo hilo hawaondoki.
"Hakuna mwananchi anayeondoka Loliondo, kinachoendelea Loliondo ni kuwa Serikali imeweka mipaka kwa kuwaongezea eneo kwa ajili ya matumizi yao ya kiuchumi", amesema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula alisema kuwa kuna utofauti mkubwa kati ya Loliondo na Ngorongoro kwani Loliondo ni eneo ambalo lilikuwa kwa ajili ya wanyama, kuzingatia mazingira na wananchi ambapo kwa sasa wananchi walihitaji kuwa na eneo zaidi la shughuli za kibinadamu na Serikali kulazimika kuweka mipaka kwenye eneo Hilo,
Aidha, Mulamula aliongeza kuwa upotoshaji unasambaa kuwa Loliondo na Ngorongoro ni maeneo ambayo yako sawa kimatumizi ambapo si kweli ndiyo maana kumekuwa na mikakati ya kuondoka watu katika hifadhi ya Ngorongoro kwa sababu wanananchi wamekuwa wengi kuliko ilivyokuwa inatakiwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kuwa Serikali imechukua jukumu la kukata eneo la Loliondo SQM 4000 ambazo zina usajili na eneo la SQM 2500 likakatwa kwa ajili ya matumizi ya Wananchi.
Masanja amesema kuwa Vyombo vya Habari vimekuwa vikipotosha kuhusu eneo hilo kwa kutaka kuharibu taswira ya wawekezaji nchini Jambo ambalo halina manufaa kwa Taifa.
"Vyombo vya Habari vinapotosha kuhusu mwekezaji aliyepo zaidi ya miaka 30 ambapo kila mwaka vitalu vya eneo hilo hutangazwa kisheria na kuingizwa katika minada ambapo mwekezaji huyo huibuka mshindi na kupata eneo lake kisheria", alisema Masanja