Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Habari ni Bidhaa ya Jamii, Sio Bidhaa ya Kuuzwa – Waziri Mkuu
May 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mawazo Kibamba – MAELEZO
Mei 28, 2022

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa leo amekutana na Waandishi wa Habari katika hafla fupi ya kutoa Tuzo za Umahiri kwa Waandishi wa Habari Tanzania katika hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam.

Tuzo hizo ni matokeo ya Mashindano yaliyofanywa kwa umoja wa Vyombo vya Habari yakijikita katika kazi za nyanja mbalimbali zikiwemo za uchumi, biashara, kilimo, utalii, haki za binadamu, utawala bora, masuala ya jinsia, watoto na walemavu, sekta ya madini, teknolojia, elimu na afya.

Kabla ya kutoa tuzo hizo Waziri Mkuu amesema tasnia ya Habari ni muhimu sana katika kuelimisha umma, na kwamba ni matarajio ya Serikali kuwa Wanahabari wote wanatafuta taarifa sahihi ili kusiwe na upotoshaji wa aina yoyote kwa wananchi, mafanikio ya nchi yetu yanawategemea wanahabari.

“Tasnia ya Habari ni muhimu sana katika kuelimisha umma hivyo, ni matarajio yetu kuwa Wanahabari wote mtatafuta taarifa sahihi ili kusiwe na upotoshaji wa aina yoyote ile,tunawategemea sana katika kuhabarisha umma wa Watanzania kuhusu mafanikio ya nchi yetu”, amesema Mhe. Majaliwa.

Amesema Serikali itaendelea na jitihada za kuhakikisha Vyombo vya Habari vinavyowahudumia wananchi kuwapa wananchi taarifa za uhakika na kwa wakati.

Mhe. Majaliwa akitoa Tuzo hizo amebainisha kwamba habari ni bidhaa ya jamii na sio bidhaa ya kuuzwa, hivyo ni wajibu kwa umma kuwahabarisha na kutetea maslahi yao.

“Mkumbuke kuwa, habari ni bidhaa ya jamii na sio bidhaa ya kuuzwa hivyo, mnawajibika kwa umma na mnapaswa kutetea maslahi ya umma” amebainisha Majaliwa.

Waziri Mkuu amemaliza kwa kuwasihi Wanahabari wote nchini kuweka kipaumbele suala la maslahi ya Taifa kwa kutumia kalamu zao vizuri katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, Nape Nnauye, ameeleza kufurahishwa kwake na kazi za Wanahabari hao katika tukio la leo, na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uamuzi wake wa kuwa karibu na Wanahabari na kutambua kazi njema inayofanywa na Wanahabari.

Nape ameahidi kuwa Wizara yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha Serikali inaweka mkono wake kuhakikisha tuzo hizo zinakuwa bora na za kudumu.

Aidha, amewahamasisha Wanahabari kushiriki katika tuzo za namna hii za kimataifa ili kulitangaza jina la nchi yetu, na hapo akawaomba ushirikiano wanahabari wote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi