Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

GCLA Yatoa Mafunzo ya Kemikali kwa Wanafunzi Mtwara
Mar 03, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Fatma Salum - GCLA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa mafunzo kuhusu matumizi salama ya kemikali kwa wanafunzi wa kidato cha tano na kidato cha sita mchepuo wa sayansi katika Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi na Sekondari ya Wasichana Mtwara zilizopo mkoani Mtwara.

Mafunzo hayo yaliyotolewa jana mkoani humo yalikusudiwa kuwapa elimu wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi likiwemo somo la Kemia ili kuwaongezea maarifa katika masuala ya kemikali ambayo ni miongoni mwa vitu wanavyotumia kujifunzia hususan kwenye maabara wakiwa shuleni.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa Kanda ya Kusini kutoka GCLA, Eliamini Mkenga aliwaeleza wanafunzi hao kuhusu Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya Mwaka 2016 ambayo inafafanua majukumu yake kuwa ni chombo cha juu na maabara ya rufaa katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba, ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali.

“GCLA inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa na wadau wote wa kemikali ndio maana tumekuja kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa sababu na nyinyi ni wadau katika matumizi ya kemikali hivyo mnapaswa kujua na kuzingatia matumizi salama ili kuepuka madhara kwa afya zenu na mazingira,” alisisitiza Mkenga.

Kwa upande mwingine Mratibu wa Ukaguzi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani na Maabara za Kemia kutoka GCLA, Magdalena Mtenga aliwaelimisha wanafunzi kuhusu kemikali hatarishi na madhara yake pamoja na hatua sahihi za kuteketeza kemikali hizo mara baada ya kumaliza kuzitumia kwenye maabara za shule. 

Mtenga alibainisha kuwa kemikali hatarishi zisipoteketezwa kwa kufuata utaratibu sahihi huweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu, wanyama na hata mimea hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuzingatia sheria, kanuni za taratibu za matumizi salama ya kemikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi, Riyadh Kadhi aliishukuru GCLA kwa kuona umuhimu wa kuwapatia wanafunzi mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuongeza uelewa katika masomo yao hasa mafunzo ya vitendo wanapokuwa maabara.

Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara, Jackson Ng’uto ameipongeza GCLA kwa jinsi walivyojipanga kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari na kutoa rai kwa mamlaka hiyo kulifanya zoezi hilo liwe endelevu hata kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kuwapa hamasa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Kwa upande wao wanafunzi waliopata mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyopata na kuiomba GCLA iendelee kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inazingatia usalama wa afya za watu na mazingira.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wadau kuhusu majukumu yake ili kurahisisha utekelezaji wa kazi zake na kusaidia jamii kwa ujumla.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi