Na Veronica Kazimoto
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Prof. Florens Luoga ameipongeza TRA kwa kukusanya kodi ya majengo kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Prof. Luoga amesema kuwa, mfumo huo umesaidia kupunguza adha kwa wananchi ambao sasa wengi wao wanatumia simu za mkononi kulipia Kodi ya Majengo badala ya kwenda kupanga foleni benki.
"Nimefurahishwa sana na uboreshaji wa mifumo ya malipo hususani katika kulipia Kodi ya Majengo ambapo watu wengi wanatumia simu zao za mkononi kulipia kodi hiyo badala ya kwenda benki kukaa kwenye foleni. Hii ni moja ya maboresho makubwa yaliyofanywa na TRA hivyo nawapongeza sana," alisema Gavana.
Gavana Luoga ameongeza kuwa, mifumo ya malipo inapoboreshwa husaidia walipakodi kulipa kodi zao kwa urahisi na kwa wakati na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla.
Aidha, Prof. Luoga ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa wakati kwa sababu maendeleo yaliyopo nchini yanatokana na kodi mbalimbali zinazolipwa na wananchi hao.
"Wito wangu kwa walipakodi na wananchi wote ni kuwasihi kuendelea kulipa kodi kwa wakati kwani faida zote wanazozipata kutokana na mfumo wa utawala waelewe kwamba umetokana na kodi mbalimbali wanazozilipa. Wanachi wanatakiwa kuelewa kwamba, upatikanaji wa elimu, maji, barabara, umeme na mambo mengine kama hayo yote yametokana na kodi," alieleza Prof. Luoga.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inashiriki maonyesho ya sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo inatoa huduma mbalimbali kama vile kusajili walipakodi, kuelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi, kutoa bili na kulipa Kodi ya Majengo.
Huduma nyingine ni pamoja na kuelezea haki na wajibu wa Mlipakodi kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma na Mlipakodi, kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya Mashine za Kielektroniki za kutolea Risti (EFDs), kuelezea mwenendo wa makusanyo ya mapato ya Serikali, na kupokea maoni, malalamiko, mrejesho pamoja na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wananchi.