Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Filamu za Tanzania Zaendelea Kung’ara Kimataifa
Oct 25, 2023
Filamu za Tanzania Zaendelea Kung’ara Kimataifa
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya Bodi ya Filamu Tanzania kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo leo jijini Dodoma.
Na Shamimu Nyaki

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea na kujadili majukumu ya Bodi ya Filamu Tanzania na kuipongeza bodi hiyo kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi za filamu hapa nchini ambayo yamesaidia kuongeza ajira kwa Watanzania.

Akiwasilisha taarifa kuhusu bodi hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema tasnia hiyo imeitangaza nchi kimataifa akizitaja filamu za Tanzania zilizofanya vizuri kuwa ni Vuta Nkuvute ya Amil Shivaji ambayo imeshinda Tuzo 14 zikiwemo za nchini Marekani na Ujerumani.

Amezitaja filamu nyingine zilizofanya vizuri kimataifa kuwa ni Jua Kali iliyofanya vizuri nchini Zambia, Binti Jasiri nchini Nigeria na Nyara nchini Nigeria.

"Bodi imeendelea kulea Wasanii na kusimamia haki zao ambapo katika malalamiko 83 yaliyopokelewa na Bodi 81 yamefanyiwa kazi, ambapo wale wanaofanya vizuri tumekuwa tukiwatunza kupitia tuzo za filamu za kila mwaka ambazo tayari zimefanyika kwa mara mbili na mwaka huu zitafanyika mwezi Novemba," amesema Mhe. Mwinjuma

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko ameitaka wizara iendelee kusimamia vyema utengenezaji wa Filamu Bora zinazoitangaza Tanzania na mandhari yake pamoja na kulinda maadili ya nchi.

Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati hiyo wakichangia taarifa hiyo kwa nyakati tofauti wameshauri Serikali iendelee kuwatambua na kuwapa nafasi Wasanii chipukizi katika majukwaa ya kimataifa pamoja na kuongeza upatikanaji wa mafunzo kwa wadau wao ili wafanye vizuri na kuhimili ushindani katika soko la kimataifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi