Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Fanyeni Kazi Kwa Bidii Huku Mkimtanguliza Mungu-Prof. Janabi
Nov 22, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amewataka wafanyakazi wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa bidii huku wakimtanguliza Mungu mbele kwani huduma wanayoitoa inagusa uhai wa  watu.

Prof. Janabi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ameyasema hayo leo wakati wa hafla fupi ya kuwaaga maafisa uuguzi wawili ambao wamestaafu kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma na kumpongeza mfanyakazi bora wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa Julai-Septemba 2018.

Alisema kazi ya kuwahudumia wagonjwa siyo kazi rahisi sana kuna wakati wagonjwa wanakuwa wakali wao na  ndugu zao jambo la muhimu ni kuwa wavumilivu na kuwahudumia kwa moyo wa upendo.

“Leo hii tunawaaga wafanyakazi wenzetu ambao wanastaafu kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma,  kazi waliyoifanya ni ngumu wanastahili pongezi. Mmoja  amefanya kazi miaka 40 na mwingine miaka 35 katika kipindi chao chote walichokuwa kazini hawakuwahi kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu”.

“Jambo la muhimu kwetu sisi tunaobaki tuwaige mfano tujitahidi kuwahi kazini , tuwepo eneo la kazi na kufanya kazi muda wote wa kazi, tushirikiane na tuheshimiane kwa kufanya hivi tutaweza kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu wa moyo”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugezi ya Huduma ya Uuguzi Robert Mallya aliwasisitiza  wauguzi hao wanaostaafu  kwenda kuwahudumia wananchi pale itakapohitajika kufanya hivyo kwani taaluma yao iko palepale na jamii inahitaji kupata huduma yao .

Akizungumza kwa niaba ya mstaafu mwenzake Afisa Muuguzi Mkuu Msaidizi Mama Agnes Mtaki aliwashukuru wafanyakazi hao kwa moyo wa upendo waliouonyesha katika kipindi chote walichofanya kazi pamoja katika Taasisi hiyo.

Mama Mtaki alisema, “Jambo la muhimu ninalowahusia ni mfanye kazi  kwa bidii huku wakimtanguliza Mungu mbele kwani huduma mnayoitoa ni ya kiroho. Kazi ya kuwahudumia wagonjwa inahitaji uvumilivu, unyenyekevu na ushirikiano”,.

Alimalizia kwa kuwataka wafayakazi hao kuheshimu kazi wanayoifanya hii ikiwa ni pamoja na kuwahi kazini,  kwani kuwa na kazi kumewafanya waheshimike, wasomeshe watoto na ndugu zao na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Wafanyakazi hao wastaafu walipewa zawadi ya mabati 100, mifuko 100 ya smenti, ngao, cheti cha kutambua kazi waliyoifanya kwa kipindi chote walichokuwa kazini  pia walikabidhiwa fedha za nauli za kurudi nyumbani kwao waliko zaliwa ambako ndiko watakapokwenda kuishi.

Mfanyakazi bora alipewa zawadi ya shilingi milioni moja, cheti cha kutambua kazi aliyoifanya  na ngao kwa ajili ya  kutoa hamasa kwa wafanyakazi wengine ili waendelee kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi