Wahandisi 17 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria kwa kukiuka maadili na taratibu za taaluma yao kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania kwa mwaka 2021 yatakayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 02 hadi 03 Septemba, 2021 katika Ukumbi wa Dkt. Jakaya Kikwete, mkoani humo.
“Wahandisi hawa 17 wamewajibishwa kwa mujibu wa makosa na adhabu wanazostahili kupewa mfano ikiwemo kujihushisha na masuala ya rushwa, upendeleo wa kazi, kushindwa kusimamia miradi na kusimamia baadhi ya miradi chini ya viwango”, amefafanua Mhandisi Barozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Prof. Bakari Mwinyiwiwa, amesema kuwa zaidi ya wahandisi 600 wanatarajiwa kula kiapo cha utii katika Maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2021 ili kuhakikisha wahandisi nchini wanawajibika vyema kwenye taaluma zao na utendaji wao wa kila siku.
Prof. Mwinyiwiwa amesisitiza kuwa kiapo kitatumika dhidi ya mhandisi atakapovunja miiko na maadili ya taaluma katika utendaji wake wa kazi na hivyo vyombo mbalimbali vya kisheria vitatumia kiapo hicho kumchukulia hatua za kisheria.
“Kiapo kinamkumbusha mhandisi kuzingatia thamani ya fedha, usalama wa maisha ya binadamu na mazingira, kutoruhusu masuala ya jinai, dini, jinsia, ukabila, rangi na masuala ya kisiasa katika utekelezaji wa kazi zao za kiuhandisi”, amefafanua Prof. Mwinyiwiwa.
Mkutano huo utakaobeba kauli mbiu ya “Athari za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda kwenye Miundombinu na Viwanda kwa Uendelevu wa Uchumi wa Kati” utashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Uganda, Misri na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao ikiwemo nchi ya Afrika Kusini, Rwanda, Botswana, DRC na Kenya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.