Na Jonas Kamaleki, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ni vema viongozi wa vyama vya siasa nchini wakaonesha mfano wa kuendesha siasa za kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha watanzania na siyo kuwatenganisha.
Ameyasema hayo leo wakati akiwasilisha Bungeni hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma
“Hivyo basi, tudumishe utulivu, amani, mshikamano pamoja na ustaarabu wetu wa Kitanzania katika kipindi chote cha kampeni na Uchaguzi Mkuu ili kulifanya Taifa letu kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.”
Aidha, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. “Hakuna kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha mifarakano.”
Waziri Mkuu amesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili linatarajiwa kuanza Aprili 5, 2020 na kukamilika Juni 26 2020.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa zoezi hilo litaenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wapiga kura katika daftari hilo. Na akatoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili waweze kutumia haki yao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020 nchini.
Amesema pamoja na mambo mengine, maandalizi hayo yanahusisha Zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika nchi nzima. Awamu ya kwanzailizinduliwa tarehe 18 Julai, 2019 Mkoani Kilimanjaro na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam.