Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Elimu kwa Umma Yasaidia Kupunguza Uvamizi wa Ardhi
Jul 27, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho.

Elimu kwa Umma inayotolewa na Serikali pamoja na Mashirika binafsi imesaidia kupunguza migogoro na uvamizi wa ardhi katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli maalum.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni mkoani Morogoro na Afisa ardhi mteule Wilaya ya Mvomero, Keneth Mwenda wakati wa mkutano mkuu wa Kijiji cha Melela kilichopo wilayani humo, uliokuwa ukipitisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi unaotekelezwa na Shirika la PELUM Tanzania.

Mwenda alisema kuwa Bajeti Kuu ya Serikali peke yake haitoshelezi kutekeleza miradi yote hivyo amewashkuru wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kujitolea kushirikiana na Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.

“Serikali kuu pekee haiwezi kutekeleza mradi wa matumizi ya ardhi kwa vijiji vyote vya wilaya ya Mvomero, ndio maana tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na shirika la PELUM Tanzania kuhakikisha vijiji vitano vya wilaya ya Mvomero vinapimwa na kupewa hati miliki,” alisema Mwenda.

Vile vile kipindi cha kiangazi wafugaji wengi huhama eneo moja kwenda lingine kutafuta malisho na matokeo yake huingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima ambayo hulimwa kwa mwaka mzima na hivyo kusababisha migogoro.

Mwenda amewaasa wananchi kuheshimu na kuzingatia mipaka ya kijiji iliyobainishwa na kuweka alama na shirika hilo pia kutii sheria ndogo ndogo zilizowekwa na wanakijiji wenyewe ili kupusha migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake Diwani wa kijiji cha Melela, Elias Lugata alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa na migogoro mingi ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima na kwamba Mpango wa Matumizi ya Ardhi utasaidia kumaliza kero zilizokuwepo kwa muda mrefu.

Nae mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Melela, Bahati Mwenyemvua alisema amefurahi kupitishwa kwa Mpango huo kwa sababu utasaidia wafugaji kutambua maeneo stahiki ya kulishia mifugo na wakulima kutambua maeneo stahiki ya kufanya kilimo.

“Wanakijiji walikuwa wanashindwa kufanya shughuli za kiuchumi kwa kukosa mikopo kutokana na kukosa kitu cha kuweka dhamana hivyo kupatikana kwa hatimiliki kutatusaidia kupata mikopo kutoka taasisi za kibenki na kuendelea kufanya shughuli nyingine za kiuchumi”, alieleza.

Kijiji cha Melela ni moja kati ya Vijiji vitano vya Wilaya ya Mvomero ambavyo vinafanyiwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi na Shirika la PELUM Tanzania ambapo jumla ya hatimiliki 500 zinatarajiwa kutolewa kwa makundi ya watu wasiojiweza kutoka vijiji vya Melela, Mlandizi, Magali, Kibaoni na Mela.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi