Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wameridhia nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Mkutano huo wa dharura wa 19 uliofanyika hivi karibuni ambao uliongozwa na Mwenyekiti, Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni pamoja na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombanza kwa niaba ya Rais Evariste Ndayishimiye huku Waziri wa masuala ya Rais, Dkt. Barnaba Marial Benjamin akimwakilisha Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.
Mkutano huo umesisitiza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa minajili ya kuimarisha maisha ya watu kupitia ushindani, kuongeza thamani za bidhaa, biashara na uwekezaji kwa uchumi endelevu.
Katika Mkutano huo, Rais Samia alisema “kulikuwa na biashara kubwa ya kubadilishana bidhaa enzi na enzi baina ya DRC na pwani ya Afrika Mashariki ikiwemo chumvi, pembe za ndovu, na dhahabu; Hivyo kuidhinisha DRC kujiunga na Jumuiya hiyo ni sawa na kurejea kwenye familia”.
Itakumbukwa kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilituma maombi ya uanachama mwaka wa 2019, ikitumai kuboresha uhusiano wa kibiashara na kisiasa na majirani zake wa Afrika Mashariki.
Fursa hiyo itawaruhusu raia wa DRC kusafiri kwa uhuru hadi nchi nyingine na biashara itakuwa ya haraka zaidi, rahisi na ya bei nafuu, ambayo inalenga kunufaisha wafanyabiashara na watumiaji wa nchi zote za EAC.
DRC ni nchi yenye watu takribani milioni 92 ambayo itakuwa ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi miongoni mwa nchi wanachama na kutaifanya EAC kuwa jumuiya yenye soko la takribani watu milioni 260; Aidha, DRC ni nchi kubwa kieneo ambayo inapakana na takribani nchi tano ambao ni wanachama wa jumuiya hiyo.