Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dola za Marekani Milioni 132 kutumika mradi mkubwa wa umeme wa upepo wa Megawati 50 Singida, Kutoa ajira 2,200.
Mar 09, 2015
Na Mhariri

[caption id="attachment_132" align="aligncenter" width="2772"]Picha Na 2 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa (katikati) akisisitiza jambo katika eneo la mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo lililopo Kisesile wilayani Singida Mjini mara kamati hiyo ilipotembelea mradi huo ili kujionea maendeleo yake pamoja na kuzungumza na watendaji wa eneo hilo.[/caption] [caption id="attachment_131" align="aligncenter" width="2772"]Picha Na 1 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa akitoa maagizo kwa Wakandarasi, Wataalamu kutoka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Wizara ya Nishati na Madini na viongozi mbalimbali kwenye majumuisho ya ziara ya kamati hiyo, baada ya kufanya ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Singida pamoja na kuzungumza na wananchi.[/caption]

Na Greyson Mwase, Singida

Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu na Nishati kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Pascal Malesa amesema kuwa serikali inatarajia kutumia   Dola za Marekani Milioni 132 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa upepo wenye uwezo wa Megawati 50 ifikapo mapema mwaka 2016.

Malesa aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ziara ya kutembelea mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo unaojengwa katika eneo la Kisesile nje kidogo ya Singida Mjini. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ipo mkoani Singida kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea maendeleo yake pamoja na kuzungumza na wananchi.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lenye asilimia 60, Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lenye asilimia 20 na kampuni ya Power Pool East Africa Limited yenye asilimia 20 chini ya kampuni ya ubia iitwayo Geo Wind Power Tanzania Limited (Geo Wind) iliyoundwa mwaka 2011.

Malesa alieleza kuwa gharama hizo zinahusisha utekelezaji wa mradi huo awamu ya kwanza kwa ajili ya kuzalisha megawati 50 ambayo itahusisha ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovolti 220 umbali wa kilomita 12 na kuunganisha kwenye gridi ya taifa.

Alisema fedha hizo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na kuongeza kuwa kwa sasa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linafuatilia mkopo huu chini ya udhamini wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha baada ya kukamilisha vigezo vyote vya mradi vilivyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kupata mkopo wa masharti nafuu na kuviwasilisha benki ya Exim ya Serikali ya watu wa China.

Alieleza kuwa baada ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya   Fedha kuwasilisha maombi ya mkopo kwenye Benki ya Exim ya China mwaka 2013, ujumbe wa kwanza kutoka benki hiyo uliwasili Tanzania mapema Machi 2014 na kufanya uhakiki wa awali wa mradi.

Alisema pamoja na uhakiki wa mradi huo, ujumbe huo ulifanya mazungumzo na Wizara ya Fedha na wanahisa wa mradi na kuongeza kuwa ujumbe wa pili kutoka Benki ya Exim ulifika Tanzania mapema Mei, 2014 na kufanya uhakiki wa kina wa mradi ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la mradi mkoani Singida na kufanya mazungumzo na uongozi wa mkoa wa Singida.

Akielezea hatua iliyofikiwa kuhusu mkopo, Malesa aliieleza kamati kuwa baada ya Serikali kupitia NDC kutimiza masharti yote ya mkopo na Benki ya Exim kutoka China kufanya uhakiki wa mradi, benki hiyo iliridhia kutolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu tangu mwezi Septemba mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu.

Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha iko katika majadiliano ya masharti ya mkopo na kusisitiza kuwa NDC inafuatilia majadiliano hayo ili kuhakikisha kuwa yanasainiwa mapema ili kuanza ujenzi mara moja ili kuendana na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao umeeleza wazi kuhusu lengo la serikali kutekeleza na kukamilika kwa mradi huu mwaka 2016.

Akielezea matarajio ya mradi huo Malesa alisema mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, mradi utaimarisha uwezo wa Gridi ya Taifa hasa wakati wa kiangazi kwa kuzalisha umeme wa uhakika na hivyo kusaidia uhifadhi bora wa maji katika bwawa la Mtera na hivyo kupunguza makali ya mgawo wa umeme nchini.

“ Mradi utalipunguzia Taifa mzigo wa kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta ya dizeli yanayotumika kwenye mitambo ya kufua umeme wa dharura”, alisema Malesa

Malesa aliongeza kuwa vilevile mradi utajenga uwezo wa kitaalam kwa watanzania kupitia progamu za kubadilishana uzoefu pamoja na ujuzi na kuongeza uhifadhi wa mazingira.

Alisema mradi utaingiza Dola za Marekani milioni 23.2 kwa mwaka kutokana na mauzo ya umeme na kutoa ajira zipatazo 2,200 na kusisitiza kuwa mradi utalipa kodi mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Pato (VAT) na nyinginezo.

Akielezea changamoto za mradi Malesa alisema ni pamoja na kuchelewa kwa upatikanaji wa mkopo kwa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ili kugharamia ujenzi wa mradi na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na Benki ya Exim kubadilisha sera za riba nafuu kutoka asilimia moja hadi mbili na muda wa mkopo kupungua kutoka miaka 25 hadi 20 huku Wizara ya Fedha ikipendelea riba kuwa asilimia moja kama ilivyokuwa awali.

Akielezea mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo Malesa alisema kuwa NDC ikishirikiana na wanahisa wenzake, inafuatilia kwa karibu sana upatikanaji wa mkopo kutoka Benki ya Exim mapema iwezekanavyo hasa ikizingatiwa kuwa mradi huu unatekelezeka kwa faida kwa kuzingatia masharti mapya ya Benki ya Exim.

Akielezea suala la fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo Malesa alisema kuwa jumla ya shilingi milioni 418 zililipwa kama fidia kwa wakazi waliopisha mradi huo katika awamu mbili tofauti.

Akielezea chagamoto wakati wa ulipaji wa fidia, Mkuu wa wilaya ya Singida Mjini anayehamishiwa katika wilaya ya Urambo Queen Mlozi, alisema wapo wakazi sita wasiokuwa waaminifu walilipwa zaidi ya mara moja huku baadhi yao wakilipwa bila kuwa na maeneo

Mlozi alisema suala la watuhumiwa hao ofisi yake imeshalikabidhi katika Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa hatua zaidi.

Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa kamati hiyo Richard Ndassa aliitaka serikali kuharakisha mchakato wa mkopo kutoka Benki ya Exim ili mradi huo uanze mara moja na mkoa wa Singida uanze kunufaika na mradi huo.

Ndasa alisema kuwa mbali na uwezo wa kuzalisha megawati 50, mradi huo una uwezo wa kuongeza hadi megati 300 kiasi ambacho ni kikubwa kwenye Gridi ya Taifa.

Alisema mbali na kupunguza tatizo la mgawo wa umeme, mradi huo pia utapelekea punguzo la bei ya umeme kutoka shilingi za kitanzania senti 30 ya awali hadi senti 13 na hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi