Na. Immaculate Makilika
Naibu waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amekitaka Chuo cha Ustawi wa Jamii kutatua changamoto zake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Hayo yamesemwa leo Chuoni hapo alipokuwa akizungumza na menejimenti, wafanyakazi pamoja na viongozi wa Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, ambapo pamoja na mambo mengine alisomewa taarifa ya maendeleo ya taasisi na mipango ya baadae.
“Nimesikia taarifa nzuri ya maendeleo na mafanikio pamoja na changamoto za Taasisi, nawaagiza viongozi kutatua changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wenu kwa kipindi cha mwezi mmoja na sisi kama serikali tutazifanyia kazi zile zinazotuhusu. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa huduma zinaendelea kutolewa kwa ubora na maslahi ya watumishi yanaboreshwa”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Pia, Naibu waziri huyo alisema kuwa anataka akabidhiwe ripoti ya utekelezaji wa utatuzi wa changamoto hizo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, kwa vile baadhi ya mambo yanahitaji ufumbuzi wa mapema ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika hiyo ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii.
Aidha, ziara hiyo ya Dkt. Ndungulie katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii ni miongoni mwa ziara za kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake katika kuboresha utendaji kazi.
Ambapo, katika kuhitimisha mkutano wake na uongozi, wafanyakazi pamoja na serikali ya wanafunzi wa Taasisi, Dkt. Ndugulile alipongeza kazi nzuri inayofanywa na watumishi na aliahidi wizara kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Ustawi wa jamii katika kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wananchi.