Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Damian Ndumbaro (MB), ameziagiza Taasisi na Mamlaka za Serikali kusogeza huduma za awali za umeme, maji, barabara na mitandao ya simu kwenye kata ya Olmoth, eneo ambalo linatarajiwa kujengwa uwanja wa mpira, kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Waziri Ndumbaro ametoa maagizo hayo, alipotembelea na kukagua eneo la ujenzi wa mradi huo, na kusema kuwa, serikali imepanga mkandarasi kuanza kazi Januari 2024, na kuwaagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), kutengeneza miundombinu ya barabara zitakazopitika wakati wote, Mamlaka za Maji kufikisha maji kwenye eneo hilo, TANESCO kufikisha umeme huku TTCL ikitakiwa kufikisha mtandao wa simu eneo hilo wenye kasi ya 5G.
Amezisisitiza taasisi hizo kufanya kazi ndani ya siku 12 zilizosalia na kukamilisha uwekaji wa huduma hizo muhimu, ambazo zitatumiwa na mkandarasi kipindi cha utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, na kuongeza kuwa mkandarasi atakapofika eneo la mradi akute tayari kuna umeme, maji na barabara zinazopitika kuingia na kutoka.
"Ninawaagiza AUWSA mkandarasi akifika akute maji, kwa ajili ya shughuli za ujenzi, fikisheni miundombinu ya maji eneo hili lote, kadhalika TANESCO leteni umeme hapa, TARURA rekebisheni barabara zote, mkandarasi atatakiwa kuleta vitendea kazi 'site' barabara za kuingia na kutoka zipitike muda wote wa utekelezaji wa mradi" amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Dkt. Ndumbaro, ameeleza kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia, ameagiza uwanja huo ujengwe Arusha, kwa lengo maalum, hivyo wananchi wa kata ya Olmoth na Arusha mmepewa heshima kubwa, shirikianeni na serikali kuhakikisha jambo hili linakamilika kwa kuzingatia maelekezo ya CAF ndani ya miezi 24, uwanja ukabidhiwe kwao, tayari kwa mashindano.
"Ujenzi wa uwanja huu, utaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya barabara nne za kuingia na kutoka, ujenzi wa viwanja vingine vitatu vya mazoezi na kimoja cha makocha, ujenzi wa maduka na migahawa ya kisasa, uwepo wa internet yenye kasi ya 5G ya bure, miundombinu ambayo itakuza hadhi ya eneo hili pamoja na Mkoa wa Arusha kwa ujumla wake,”amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Hata hivyo amewapongeza wananchi wa Arusha, kwa kukubali uwepo wa ujenzi huo, eneo hilo na kuwakumbusha kuwa, wanayo bahati kuwa wenyeji wa mashindano na kuwa uwanja huo, ungeweza kujengwa mkoa wowote Tanzania, kuchaguliwa Arusha kata ya Olmoth, wananchi hao wanapaswa kushukuru, kuheshimu na kuthamini maamuzi hayo ya serikali.
Awali ziara hiyo iliambatana na makabidhiano ya Hati Miliki ya eneo hilo, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, amemkabidhi Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Hati Miliki ya Eka 39 za awali.