Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt Nchimbi Atoa Mwezi Mmoja kwa Halmashauri ya Iramba Kujenga Vyoo Mnada wa Malendi.
Oct 31, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu - Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amempa mwezi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni kujenga vyoo bora katika Mnada uliopo Kijiji cha Malendi, Kata ya Mgongo Wilayani humo..

Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea mnada huo ambapo wananchi wamelalamika kukosa huduma za vyoo na maji kwa kipindi kirefu huku halmashauri hiyo ikiendelea kukusanya ushuru bila kuwaboreshea miundombinu.

“Mkurugenzi nakupa mwezi mmoja hapa kuwe na vyoo bora vikiwa na matundu sita kwa ajili ya wananchi hawa pamoja na huduma za maji kwani kipindi cha mvua kinaanza hivyo lazma muwajali wananchi hawa kwa kuwa kipindupindu kinaweza kulipuka hapa”, ameeleza Dkt Nchimbi.

Ameongeza kuwa kwa kuwa hakuna vyoo wananchi watajisaidia maeneo ya jirani na mnada na mvua zikianza zitatiririsha uchafu huo katika eneo la mnada na makazi ya wanakijiji cha Malendi na hivyo kusababisha milipuko wa magonjwa hasa Kipindupindu.

Dkt Nchimbi amesema Mkurugenzi huyo ajenge vyoo vyenye matundu sita pamoja na kuvuta huduma za maji kwakuwa maji husaidia usafi wa eneo hilo na kupunguza uwezekano wa magonjwa hayo.

“Halmashauri mna jukumu la kuhakikisha mnada huu una miundombinu yote hasa ya maji na vyoo kwakuwa mnakusanya ushuru pia kumbukeni kuhakikisha huduma zinapatikana vizuri mnadani hapa”, ameelekeza Dkt Nchimbi.

Aidha amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na idara za usafi wa mazingira na Wakala wa Barabara vijijini (TARURA) wanahakiki njia na mitaro ya kupitisha maji ili mvua zisilete maafa pamoja na kuhakiki mabwawa ili baada ya mvua kuisha waweze kuvuna maji ya kutosha.

Dkt Nchimbi ameeleza kuwa mvua za msimu uliopita zilileta maafa ya kipindupindu hivyo hatarajii kwa mvua za msimu huu kuleta tena magonjwa kwakuwa wakurugenzi wametahadharishwa mapema uwepo wa mvua za wastani na juu ya wastani.

Amewashauri wananchi kuimarisha makazi yao ili yaweze kuhimili mvua hizo pamoja na kujenga vyoo bora ili wasipate magonjwa ya kuambukiza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Marietha Kasongo amesema amelipokea agizo hilo na kuongeza kuwa mwezi mmoja unatosha kujenga vyoo hivyo na kufikisha huduma za maji mnadani hapo.

Amesema halmashauri ilikuwa na mpango wa kujenga vyoo na kuvuta maji mnadani hapo hivyo agizo la Mkuu wa Mkoa limewaamsha ili waweze kutekeleza mipango yao kwa haraka zaidi.

Awali Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetangaza kuwa Mkoa wa Singida unatarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani, aidha wastani wa mvua kwa Mkoa wa Singida ulikuwa ni Milimita 500 mpaka 850.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi