Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Nchemba Ateta na Balozi wa Denmark Nchini Tanzania
Mar 18, 2024
Dkt. Nchemba Ateta na Balozi wa Denmark Nchini Tanzania
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa Mkutano na Balozi wa Denmark hapa nchini, Mhe. Mette Dissing-Spandet (hayupo pichani) ambapo ameishukuru nchi hiyo kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha jijini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameishukuru Denmark kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida.

 

Dkt. Nchemba ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mheshimiwa Mette Dissing-Spandet, ofisini kwake Jijini Dodoma ambapo walijadili masuala kadhaa ya ushirikiano.

 

Alisema kuwa uhusiano wa Tanzania na Denmark umetimiza miaka 60 na katika kipindi hicho, nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na kiuchumi ambapo hivi karibuni nchi hizo zilikuwa zikitekeleza miradi ambayo Denmark iliipatia Tanzania msaada wa takriban Denish Krone bilioni 2 sawa na shilingi bilioni 646.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing-Spandet akizungumza wakati wa mkutano wake na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ambapo alisema kuwa nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika eneo la nishati jadidifu, pamoja na gesi na kusaidia kukuza sekta binafsi ili iweze kuchangia maendeleo ya nchi. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.
 

Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (DANIDA) imetoa zaidi ya shilingi bilioni 103 zinazotokana na mapato ya uwekezaji wake wa hisa katika Benki ya CRDB, ambazo zimetumika kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya.

 

Aidha, aliipongeza Denmark kwa kusitisha uamuzi wake wa kutaka kufunga Ubalozi wake hapa nchini na kwamba hatua hiyo itaimarisha zaidi ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Denmark kupitia mpango wake mpya wa ushirikiano baada ya kusitisha uamuzi huo wa kufunga ubalozi wake nchini ambapo nchi hiyo imepanga kuongeza kiwango cha ufadhili na kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo yatakayokuza uchumi, ikiwemo nishati, kuboresha mifuko ya kodi, kilimo, elimu, afya, pamoja na kusaidia sekta binafsi.

 

Dkt. Nchemba pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Denmark kuja kuwekeza mitaji yao hapa nchini ikiwemo sekta ya fedha na kunufaika na vivutio vilivyowekwa na Serikali baada ya kurekebisha sheria kadhaa, lakini pia kunufaika na soko la uhakika linalopatikana katika nchi za SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kulia), ukiwa katika mkutano na ujumbe kutoka ubalozi wa Denmark nchini ukiongozwa na Balozi wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, Jijini Dodoma.

Aliiomba pia Denmark kupitia Taasisi yake inayohusika na masuala ya Bima na Dhamana (Danish Export Credit Agency), kushiriki katika ujenzi wa mradi wa SGR kwa vipande vilivyobaki kutokana na umuhimu wa mradi huo katika kukuza biashara na ustawi wa maisha ya watu watakaotumia reli hiyo pamoja na kukuza pato la Taifa.

Kwa upande wake, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mheshimiwa Mette Dissing-Spandet alisema kuwa nchi yake inapongeza mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea hivi sasa na kwamba iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mheshimiwa Spandet alisema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika eneo la nishati jadidifu, pamoja na gesi na kusaidia kukuza sekta binafsi ili iweze kuchangia maendeleo ya nchi.

Alisema kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo Kimataifa, Mhe. Dan Jorgensen, anatarajia kufanya ziara rasmi ya kikazi hapa nchini mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ambapo atatumia ziara hiyo kujadiliana na Serikali maeneo ya kipaumbele ambayo nchi hizo zitajielekeza katika mpango huo mpya wa ushirikiano.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi