Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu huku akisisitiza kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu na kwa umakini suala la upatikanaji wa mafuta nchini ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji na usafirishaji haziathiriki.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mvumi Mission, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma, Dkt. Nchemba amesema Serikali inaendelea kufanya vikao vya mara kwa mara na wadau mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa hiyo muhimu haipatikani kwa shida.
“Niwahakikishie kuwa Serikali inafuatilia suala hili kwa karibu. Kila siku tunafanya vikao vya sekta mbalimbali kuhakikisha mafuta hayaadimiki na tunashughulikia pia masuala ya bei ya bidhaa na huduma,” amesema Dkt. Nchemba.

Ameeleza kuwa upatikanaji wa mafuta si suala la kuamuliwa na nchi moja pekee, kwani kuna nchi zinazozalisha na nyingine kuagiza, hali inayofanya mnyororo wa upatikanaji wake kuathiriwa na changamoto za kimataifa, ikiwemo migogoro ya vita.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inalenga kulinda maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanapata bidhaa hiyo kwa bei nafuu na kuweza kuendelea na shughuli zao za kila siku bila usumbufu.
Ameongeza kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kufanya tathmini ya kina kwa kushirikiana na watoa huduma ili kupata suluhisho la kudumu bila kuleta taharuki kwa wananchi.

Dkt. Nchemba amekumbusha kuwa hali kama hiyo iliwahi kutokea hapo awali na Taifa liliweza kuvuka salama kutokana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kusisitiza kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha upatikanaji wa mafuta hauathiri ukuaji wa uchumi wa nchi.