Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mwigulu Awataka Vijana Wahitimu Kuchangamkia Fursa za Kiuchumi na Maendeleo
Dec 11, 2023
Dkt. Mwigulu Awataka Vijana Wahitimu Kuchangamkia Fursa za Kiuchumi na Maendeleo
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza wakati wa hafla ya Mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, duru ya pili, Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza.
Na Eva Ngowi na Ramadhani Kissimba, Mwanza

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Waziri wa Fedha katika Mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya ziwa - Mwanza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, aliwataka wahitimu hao kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza kutokana na mazingira yanayotengenezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

‘Miongoni mwa fursa hizo ambazo nilisisitiza pia kwenye duru ya kwanza ya mahafali haya huko Dodoma ni kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine’ alisema Bi. Omolo

 

Aidha Bi. Omolo alisema kuwa ulimwengu wa sasa umebadilika na kuna fursa nyingi ndani na nje ya nchi, hivyo kuwataka vijana kuchangamkia kila fursa inayojitokeza mbele yao.

 

Bi. Omolo aliwataka vijana kote nchini kuimarisha ushirikiano hasa kwa vijana ambao kwa njia moja au nyingine hawakubahatika kupata maarifa na ujuzi na kuwataka vijana wasomi kutowatenga wenzao bali wawafanye kuwa sehemu yao maana kwa kufanya hivyo itakuwa chachu ya kutoa mchango wa kukabiliana na changamoto za maendeleo zinazoikabili jamii.

Aidha, Bi. Omolo alikipongeza Chuo hicho kwa mafanikio iliyoyafikia, na pia kwa kushika nafasi ya kwanza kwa utendaji bora katika usimamizi wa rasilimali watu na utawala bora kwa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu nchini, tuzo ambayo ilitolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mwezi Oktoba, 2023.

 

Awali Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen Mayaya, alisema kuwa chuo chake kimeendelea kupokea kwa wakati fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayojengwa kwa kasi katika Chuo hicho hali inayosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Taasisi  kukuza taaluma ya Wanamipango nchini.

 

Profesa Mayaya aliongeza kuwa, Chuo hicho kitaendelea kujizatiti katika kuwandaa wataalamu wenye weledi wa kutosha katika fani za mipango ya maendeleo na kutoa wataalamu wenye uzalendo na waadilifu kwa kuwa uzalendo na uadilifu ndizo nyenzo muhimu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.


Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, CPA, Dkt. Samwel Werema, alisema kuwa Uongozi wa Chuo  hicho utaendelea kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi wa hali ya juu ili kusimamia dhamana iliyopewa ya kusimamia Chuo na hasa ikizingatiwa kuwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ndio Chuo pekee nchini chenye jukumu la kuandaa wataalam wa mipango ya maendeleo.

 

Dkt. Werema, aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha mageuzi ya kiuchumi, watalaam wa mipango wanahitajika kwa wingi, na Chuo kimejizatiti katika kuzalisha watalaam hao ili waende kusaidia kuongoza shughuli za maendeleo zitakazokuza uchumi wa nchi.

 

Mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa – Mwanza yanafanyika kwa mara ya 11 ikijumuisha wahitimu 2618 wakiwemo wanaume 1211 na wanawake 1407 ambao wametunikiwa tuzo katika programu ya Astashada, Stashahada na Shahada.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi