Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mwigulu Akutana na Wawekezaji wa Ufaransa
May 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eva Ngowi, WFM, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi kutoka Ufaransa (MEDEF) na Taasisi ya Biashara ya Ufaransa, kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo cha mafuta ya kula.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam, alipokuna na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirikisho hilo unaouhusisha kampuni 41 uliopo nchini kwa mwaliko wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alioutoa wakati wa ziara yake aliyoifanya nchini Ufaransa hivi karibuni.

Dkt. Nchemba alisema kuwa nchi inakabiliwa na uhaba wa mafuta ya kula kutokana na uzalishaji mdogo wa alizeti na mawese pamoja na athari za vita baina ya Urusi na Ukraine, vilivyosababisha bei ya mafuta kupanda na kwamba Serikali iko tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kilimo hicho.  

 “Kwa kuzingatia hali iliyotokea duniani baada ya uviko 19 na haya ambayo yanaendelea ya mzozo wa nchi mbili, Urusi na Ukrein, ambao ni wazalishaji wakubwa wa mafuta ya kula, nitoe wito kwa wawekezaji kuwa Tanzania inaweza kulisha dunia kwa suala la mafuta ya kula mkiwekeza kwenye eneo hilo” alisema Dkt. Nchemba

Alisema kuwa kuna mikoa zaidi ya nane inayofaa kwa uzalishaji wa mafuta ya alizeti na mikoa mingine zaidi ya minne inayofaa kwa kilimo cha mawese na kuwaalika wawekezaji hao kuchangamkia fursa hiyo ili kutosheleza soko la ndani na kuilisha dunia.

“Nchi ambazo zinazalisha sana mafuta ya kula, ukizilinganisha kwa fursa, hazijaifikia Tanzania; kwa hiyo tunachohitaji ni uwekezaji ili tuweze kufidia pengo lililopo katika dunia kwa sasa la upatikanaji wa mafuta ya kula” alisisitiza Mhe. Dkt. Nchemba. 

Alitoa wito kwa wawekezaji hao kutoka Ufaransa kushirikiana na  kukutana na sekta binafsi ya Tanzania ili kungalia maeneo ya kuwekeza pia kwa pamoja na kwamba Serikali iko tayari kutoa ushirikiano wa kila hali ili kufaninikisha uwekezaji wao katika sekta mbalimbali walizojipanga kuja kuwekeza.

“Sisi Wizara ya Fedha na Mipango tumeifanyia kazi changamoto ya utozaji kodi mara mbili na suala hilo liko hatua za mwisho za maamuzi, na tutatekeleza nyenzo ya blue print ili kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji na kufanyia biashara; tunawahakikishia kwamba tutashirikiana na sekta binafsi kwa sababu sekta hiyo ndio injini ya kukua kwa uchumi” aliongeza Dkt. Nchemba. 

Dkt. Nchemba, alisisitiza kuwa wawekezaji kutoka Ufaransa na kwingineko wanakaribishwa kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali kwa sababu kuna fursa nyingi za uwekezaji katika kilimo lakini pia katika sekta nyingine kama vile ujenzi wa miundombinu, maliasili, bandari, uvuvi na usafirishaji na kwamba kuna soko la uhakika hapa nchini, Afrika Mashariki na nchi za SADC, hatua itakayosaidia pia kukuza ajira kwa vijana.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa aliyeambatana na ujumbe huo, Mhe. Samuel Shelukindo, alisema kuwa wawekezaji hao wameona fursa kubwa ya kuwekeza katika nyanja mbalimbali na kwamba wako tayari kuwashawishi wawekezaji wengine kuja kutafuta fursa hiyo ikiwemo sekta ya kilimo cha uzalishaji wa mafuta ya kula.

 “Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara ya kikazi nchini Ufaransa tarehe 10 hadi 14 mwezi Februari mwaka huu na alikutana na wafanya biashara na wawekezaji ambapo katika mazungumzo yao aliwakaribisha Tanzania ili waangalie maeneo ya uwekezaji na kufanya biashara. Ujumbe huu mkubwa wa takribani makampuni 40 wamekuja kwa ajili ya kuitikia wito huo” alisema Mhe. Balozi Shelukindo.

Kwa Upande wa Makamu Mwenyekiti wa Ujumbe wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi ya Ufaransa (MEDEF) na Taasisi ya Biashara ya Ufaransa, Bw. Gerard Wolf, alisema wamekuwa na mazungumzo na Mawaziri wa Sekta mbalimbali na kwamba wako tayari kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania likiwemo eneo la uchumi wa bluu, sekta ambayo alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa nchini kwao. 

Alizitaja sekta nyingine ambazo Shirikisho hilo limevutiwa nazo kuja kuwekeza kuwa ni nishati, maji, ujenzi wa miundombinu, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na kilimo na kuahidi kuwa watapeleka ujumbe kwa kampuni nyingine zaidi ili zije kuwekeza kwenye kilimo cha alizeti na michikichi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi