Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Kufungua Mashindano ya SHIMUTA Tanga Novemba 21, 2022
Nov 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Oscar Assenga, TANGA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafasi nchini (SHIMUTA) Novemba 21 mwaka huu kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Hayo yalibainishwa leo na Mwenyekiti wa SHIMUTA Taifa, Roselyne Massam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani Tanga kuhusu mashndano hayo ambapo alisema kwa mara ya kwanza tokea yalipoanza mwaka huu 2022 yameweka rekodi mpya.


Alisema rekodi hiyo inatokana na kuongezeka kwa idadi ya timu na sasa kufikia 52 zitakazochukua kuwasaka mabingwa kupitia michezo watakayoshindaniwa ambayo itatimua vumbi leo Novemba 15 katika viwanja mbalimbali Jijini hapa

Mwenyekiti huyo alisema tangu wameshika hatamu ya kuliongoza shirikisho hilo haijawahi kutokea kushirikisha timu nyingi zaidi kama mwaka huu jambo ambalo linaonyesha mwitikio kuwa mkubwa na michezo hiyo kuonekana kuleta tija kwa washiriki mashirika, makampuni na taasisi zenyewe wanazotoka.

Naye kwa upande wake Mratibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Maswet Masinde alieleza namna walivyojipanga kuhakikisha hakuna mamluki atakayechezeshwa kwenye timu zitakazoshiriki mashindano hayo kwani wamejipanga kusimamia sheria kanuni na taratibu zinazowaongoza katika michezo yote.

Mashinde alisema kwamba msimu huu wamekuwa wakali zaidi kuhakikisha wanadhibiti mamluki hivyo wamekwisha kufanya uhakiki kuondoa mamluki kwa kutumia taasisi za umma ikiwemo NHIF, WCF, PSSF kuhakiki washiriki lengo likiwa ni michezo hii iwe ni kwa ajili ya watumishi wale ambao wanatambulika kisheria na ili uwe mshiriki unapewa leseni maalumu na lazima uwe umehakikiwa kwenye mifuko hiyo.

Mratibu huyo alisema kwamba mpaka sasa wanamichezo 2,183 ambao tayari wameshafika hapa jijini Tanga na ni namba kubwa ya wanamichezo wanaoshiriki lakini tuna kanuni ambazo zinaongoza mashindano pia watatumia kanuni za michezo husika pale inapobidi huku akisisitiza umuhimu wa waamuzi wasimamie sheria taratibu na miongozo inayoongoza michezo husika ili kusiwepo na manung'uniko ya hapa na pale


Akieleza namna mkoa huo ulivyojipanga kuelekea Mashindano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba amesema kwamba mkoa upo salama na kuwahakikishia ulinzi na usalama muda wowote watakapokuwepo kwenye mashindano hayo.

Mkuu huyo wa Mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wakazi wa Tanga wakiwemo wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo kuchangamkia fursa za uwepo wa mashindano hayo kujiongezea kipato.

"Mashindano haya ni zaidi ya michezo yana faida ya kipato lakini yanainua uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuongeza Pato la Taifa, nitoe wito kwa wafanyabiashara wote kuchangamkia fursa na kujitokeza kwa wingi katika michezo hii", alisema Mgumba.

"Suala la hali ya ulinzi na usalama liko vizuri, tumeendelea kuimarisha doria kwa sababu tumepata ujio wa watu wengi, hivyo hali ya usalama iko vizuri tumeendelea kujiimarisha zaidi doria za mchana na usiku kuwahakikishia wanamichezo na wageni wetu wote wanakuwa salama wakati na hata baada ya kumaliza michezo", aliongeza.

Michezo itakayochezwa wakati wa mashindano hayo ni michezo ya mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete, wavu, kikapu, dats, pool table, vishale, draft, kukimbia kwa magunia, riadha, kuvuta kamba, bao na mingineyo kedekede, lengo kuu hasa ikiwa ni kuimarisha mahusiano baina ya taasisi, mashirika na makampuni kuimarisha afya kupitia michezo ikiwa pia ni kuondokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Michezo hiyo ambayo hufanyika kila mwaka ni kwa mara ya pili mfululizo kufanyika ndani ya mkoa huo kwa mwaka huu yakija na kauli mbiu ya 'SHIMUTA familia moja'.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi