Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Azindua Mpango Jumuishi Wahudumu Afya Ngazi ya Jamii
Jan 31, 2024
Dkt. Mpango Azindua  Mpango Jumuishi Wahudumu Afya Ngazi ya Jamii
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezielekeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Mamlaka nyingine zinazohusika kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili uweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Amesema ni lazima kuweka mfumo mzuri wa uratibu wa shughuli za mpango huo na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana ikiwemo kutumia mifano ya kidijitali.

Makamu wa Rais amewasihi wahudumu wa afya watakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hilo kuzingatia weledi na kujituma pamoja na kutoa rai kwa jamii kuupokea mpango huo na kuthamini huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha afya katika jamii.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza masuala ya lishe bora na usafi wa mazingira yasiachwe nyuma katika kutekeleza Mpango huo kama njia mojawapo ya kujenga afya na kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na uchafuzi wa mazingira ikiwemo kipindupindu na malaria.

Ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali pamoja na vipaumbele vya Mpango huo vilivyoainishwa wakati wote wa utekelezaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi