Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amefungua jengo la makazi la kibiashara na kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kuziwezesha Taasisi zake kuwa na miradi mikubwa itakayoziwezesha kujitegemea.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo la makazi la kibiashara lililopo Kata ya Sekei jijini Arusha, Dkt. Mpango amesema Serikali imeiruhusu Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kushirikiana na sekta binafsi kwa ubia ili kuiwezesha kutekekeza miradi ya kimkakati na itakayoleta tija haraka na hivyo kupunguza utegemezi wake kwa Serikali.
“Nawapongeza kwa ujenzi wa jengo zuri la kisasa, endeleeni na mpango wa kujenga majengo ya aina hii katika maeneo mbalimbali ya kimkakati yatakayowezesha kuhudumia kaya nyingi na zingatieni uhifadhi wa mazingira na kwa kupanda miti na maua na kuweka mifumo mizuri ya kuondosha takataka”, amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango ameitaka TBA kufanya uwekezaji wenye tija katika maeneo yake na kuhakikisha wapangaji wa majengo yake wanalipa kodi kwa wakati.
Ameitaka Wizara ya Uwekezaji kuhakikisha inaweka msukumo kwenye ujenzi wa viwanda vya vifaa vya ujenzi ili kupunguza gharama za ujenzi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la ujenzi wa nyumba nyingi zitakazokidhi mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu.
“Serikali imedhamiria kukuza sekta ya nyumba ili ichangie Pato la Taifa na hivyo kukuza uchumi”, amesisitiza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa azma ya ujenzi huo ni chimbuko la TBA la kutaka kujiendesha kibiashara na hivyo kupata faida.
"Mfumo wa kisasa wa vitasa janja ili kudhibiti wapangaji wenye madeni na hivyo kusaidia ulipaji wa kodi kwa muda muafaka, lengo ni TBA kupata mapato zaidi na kujiendesha yenyewe", amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula, ameipongeza TBA kwa kujenga majengo marefu yanayohudumia idadi kubwa ya watu na kusisitiza kuwa majengo hayo yaendane na uwepo na maegesho ya magari.
Amesisitiza kuwa mahitaji ya nyumba nchini zaidi ya 390,981 kwa mwaka wakati nyumba zinazojengwa na taasisi mbalimbali kwa mwaka ni chini ya 2,000, hivyo amewataka wadau mbalimbali wa ujenzi waendelee kujenga nyumba ili kuendana na ongezeko la idadi ya watu ambapo inakadiriwa takriban watu zaidi ya milioni 1.6 wanaongezeka kila mwaka.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema jengo hilo lenye sakafu 11 limeongeza thamani ya Mji wa Arusha hususan kipindi hiki ambacho idadi ya watalii imeongeza na hivyo kuchochea shughuli za biashara katikati ya jiji.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TBA, Msanifu Majengo Daud Kondoro amesema kukamilika kwa mradi huo utawezesha Wakala kujenga majengo mengine marefu ya makazi na biashara katika eneo la Sekei ili kuhamasisha shughuli za Utalii katika jiji hilo.
"Tumejipanga kuhakikisha miradi ya makazi na biashara iliyoko Canadian - Masaki, jijini Dar es Salaam, Ghana Kotta jijini Mwanza, Tameke Kotta na nyumba 150 (Awamu ya Pili) eneo la Nzunguni jijini Dodoma inakamilika ili kuiwezesha TBA kuondokana na utegemezi kwa Serikali”, amefafanua Kondoro.
Jengo la makazi la kibiashara eneo la Sekei lenye sakafu 11 lina uwezo wa kuhudumia kaya 22 na limegharimu zaidi ya shilingi bilioni 6.8 ambapo ujenzi wake umetekelezwa katika awamu nne.