Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 18 Oktoba 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano imara uliopo tangu Tanzania ilipopata Uhuru mwaka 1961. Amesema Tanzania inatambua mchango wa Japan katika kuunga mkono juhudi za maendeleo hususani katika ujenzi wa miundombinu, maji, sekta ya elimu pamoja na masuala mbalimbali ya ushirikiano.
Makamu wa Rais amesema kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD), Tanzania imenufaika kupitia programu mbalimbali na dhamira ya serikali ni kuendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya Japan kwa manufaa ya pande zote mbili.
Makamu wa Rais amesisitiza kuimarishwa ushirikiano zaidi wa Tanzania na Japan katika biashara, uwekezaji, utalii, matibabu ya kibingwa, mafunzo katika utalaamu na ubobezi wa masuala ya afya pamoja na vifaa tiba na dawa. Pia ametaja maeneo mengine ya ushirikiano ikiwemo uhifadhi wa mazingira, utaalamu katika biashara ya kaboni pamoja na teknolojia bora katika sekta ya uchumi wa buluu.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa amesema katika kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya mataifa haya mawili, tayari yameanzishwa majadiliano ya kibiashara baina ya Tanzania na Japan (Bilateral Bussiness Dialogue) kwa lengo la kuimarisha biashara kwa pande zote mbili.
Ameongeza kwamba, Japan imeendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya Afya ikiwemo shirika binafsi la TOKUSHUKAI MEDICAL GROUP ambalo limekuwa likishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na pia limeweza kuijengea uwezo Hospitali ya Benjamin Mkapa kufanya huduma ya upandikizaji figo. Pia amesema ipo dhamira ya ujenzi wa kituo cha matibabu ya figo kitakachoweza kusaidia mikoa mbalimbali pamoja na nchi za Jirani pamoja na uwekezaji katika matibabu ya kibingwa ya upasuaji ubongo (Neurosurgery).
Aidha, Balozi Misawa amesema Japan itaendelea kuwa mdau wa utalii nchini Tanzania ambapo idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wanadhamiria kutembelea na kupanda mlima Kilimanjaro.