Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mollel: Wataalamu wa Afya tengeni Muda Kutembelea Vivutio vya Utalii Nchini
Dec 27, 2023
Dkt. Mollel: Wataalamu wa Afya tengeni Muda Kutembelea Vivutio vya Utalii Nchini
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya utalii wa ndani wa kuwalisha wanyama walipotembelea shamba la wanyamapori la Serval Wildlife Siha llililopo wilayani Siha. Wataalamu wa JKCI walikuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Na Mwandishi Maalumu –Siha

Wataalamu wa afya nchini wametakiwa kutenga muda wa kufanya utalii wa ndani kipindi wanachokuwa likizo ili kujionea vivutio mbambalimbali vilivyopo kwa kufanya hivyo kutasaidia kupumzisha akili zao.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha, Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu utalii tiba unavyoendana na utalii wa vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Mhe. Dkt. Mollel ambaye aliambatana na wataalamu wa Taasisisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutembelea shamba la wanyamapori Serval Wildlife lililopo wilayani Siha kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani.

Alisema wataalamu wa afya wanafanya kazi kubwa na ngumu ya kuokoa maisha ya wagonjwa hivyo basi ni muhimu kipindi wanapokuwa likizo wakatenga muda wa kupumzisha akili zao kwa kutembellea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kwani kwa kufanya hivyo wataweza kufanya kazi zao vizuri Zaidi.

“Leo nimekuja hapa kuwapa zawadi wataalamu wa JKCI waliyopewa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, zawadi hii tumewapa baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha miundombinu ya afya alisema tuanze kufanya utalii tiba na taasisi ya kwanza kuelewa hili jambo na kuanza kulitekeleza ni JKCI na wengine wakafuata”,

“Nimekuja hapa kuwaonesha jinsi utalii tiba unavyoendana na utalii wa kawaida wameona utalii uliopo kwa kujua kwao kutasaidia kuwajulisha wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaowatibu kuwahamasisha kutembelea vivutio vilivyopo pindi watakapoona”, alisisitiza Mhe.Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Fawad Hamoud, Mkurugenzi Mtendaji wa shamba la wanyamapori la Serval Wildlife aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kutembelea shamba hilo na kusema kuwa JKCI imekuwa  ni taasisi ya kwanza kutembelea mahali hapo na kupata nafasi ya kulisha wanyama na kupiga nao picha.

Fawad alisema katika shamba hilo wanajishughulisha na ufugaji wa wanyamapori ambao ni tofauti na ufugaji wa wanyama wengine walioko Zoo kwani ukiwa katika shamba hilo unakaa karibu na wanyama akiwemo simba unawalisha chakula na kupiga nao picha.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutupa nafasi ya kufanya uwekezaji mahali hapa na tunatumia nafasi hii kutangaza utalii, tunapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuona wanyama, tunawaomba wananchi mje mahali hapa kulisha wanyama na kupiga nao picha”, alisema Fawad.

Nao wafanyakazi wa JKCI waliotembelea vivutio hivyo walimshukuru Waziri wa Afya kwa kuwapa nafasi hiyo na kusema kuwa wameona utalii uliopo na hiyo itawasaidia kutangaza vivutio hivyo kwa wagonjwa wanaowatibu pamoja na wataalamu wa afya wanaokuja kufanya kambi za upasuaji wa moyo kutoka nje ya nchi.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walikuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi na kutumia nafasi hiyo kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo katika wilaya hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi