Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mkama: Wafundisheni Wengine Kutengeneza Majiko Banifu
Jul 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama ametoa rai kwa kaya zilizotengeneza majiko banifu kusambaza maarifa hayo kwenye kaya zingine ili kusaidia kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Ametoa rai hiyo alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika vijiji vya Kiloleli, Beledi na Mihama wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanavikundi vinavyonufaika na mradi huo, Dkt. Mkama aliwataka watumie maarifa waliyopata katika utengenezaji wa majiko hayo rafiki wa mazingira kuwafundisha wengine hatua itakayosaidia kupunguza ukataji miti.

“Niwapongeze kwa kuibeba wilaya katika utengenezaji wa majiko, huu utaalamu wenu muwarithishe wengine na watahamasika mpaka wote watahama kutoka kwenye kukata miti kwa ajili ya kuni hivyo watahamia kwenye majiko,” alisema.

Pia, Naibu Katibu Mkuu huyo aliwapa tahadhari wananchi hao kuwa ukataji miti unasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha upungufu wa mvua.

Aliongeza kuwa miradi hiyo inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa na msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto za kimazingira, hivyo wananchi wanapaswa kuilinda.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mkama alisema changamoto ya uhaba wa maji katika vijiji hivyo itakuwa historia baada ya kukamilika kwa uchimbaji wa malambo matatu.

Aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanayatunza malambo hayo ikiwemo kuyaweka katika hali ya usafi na kuepuka kufanya shughuli zisizotakiwa zikiwemo kufua au kuogelea, pindi uchimbaji wake utakapokamilika.

Wakitoa maoni kuhusu mradi huo, Bi. Paulina Selia na Emmanuel Masanja ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Beledi aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapelekea mradi katika kijiji chao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi