Na Thobias Robert
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inatambua mchango wa Umoja wa mataifa na itaendelea kushirikiana na umoja huo katika kuleta maendeleo, kulinda amani, kusaidia wakimbizi pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchni.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sherehe ya maadhimisho ya miaka 72 ya Umoja wa Mataifa ambayo hapa nchini yatakayofanyika Oktoba 24, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee.
Dkt. Kolimba alisema kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa ni washirika wakubwa katika kusimamia na kufadhili miradi ya maendeleo ikiwemo maji, elimu nishati, miradi ya ujenzi wa miundombinu, kufadhili na kuwahudumia wakimbizi waishio maeneo ya mipakani kutoka mataifa jirani, kwahiyo uwepo wao hapa nchini una muhimu mkubwa.
“Kwa sasa Tanzania inashirikiana na kusaidiana na umoja wa mataifa katika mambo ya kulinda amani, kudumisha umoja, lakini pia kuendeleza maendeleo endelevu hususani shughuli za kiuchumi hapa nchini,” alifafanua Dkt. Kolimba.
Aidha aliendelea kusema kuwa, Umoja wa Mataifa imekuwa ikisaidia mikoa ambayo ipo karibu na mipaka ya nchi za nje hususani mikoa inayohifadhi wakimbizi katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi, ili iweze kuwasaidia wakimbizi wengi wanaokuja hapa nchini.
“Umoja wa Mataifa kwa kupitia taasisi zake mbalimbali katika malengo yao 17 uliyojiwekea, yamegusa pia katika sekta ua elimu katika shule za msingi na sekondari kwa kujengewa vyoo, kujenga vituo vya afya, vifaa vya maabara, vilevile kuna baadhi ya barabara zimejengwa kwa msaada Umoja wa Mataifa,” alieleza Dkt. Kolimba.
Aliendelea kusema kuwa, mwaka huu Umoja wa Mataifa umetoa zaidi ya shilingi milioni 220 katika Chuo cha Polisi mkoani kilimanjaro ili kuwajengea uwezo walimu na askari wa chuo hicho katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wananwake.
Kwa upande wake Mratibu Mkaazi Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez amesema Tanzania inapita katika mabadiliko ya kisera na kiuchumi ili kujenga maisha bora ya Wananchi wake hivyo Umoja huo utaendelea kuisaida juhudi hizo ili Tanzania itimize ndoto ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Sisi kama Umoja wa Mataifa tunaendelea kufanya kazi na serikali ya Tanzania ili kuleta maendeleo, pia tunaipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwahifadhi wakimbizi wengi kutoka mataifa ya nje, tuatendelea kushirikiana na watanzania na wadua mablimbali katika kuleta maendeleo hapa Tanzania,” alisistiza Bw, Rodriguez.
Aidha aliongeza kuwa, matatizo yanayoikumba Tanzania kama vile magonjwa ya mlipuko, mabadiliko ya tabia ya nchi, wakimbizi, hayawezi kutatuliwa nan chi peke yake bali kwa kushirikiana na wadau kikanda, kijumuia pamoja kimataifa ili kuendeleza na kutimiza malengo ya 17 maendeleo endelevu (Sustainable Develepment Goals) kama ilivyoazimiwa na nchi wa wanachama wa umoja huo.
Kwa sasa umoja wa mataifa unatekeleza mikakati miwili hapa nchini ikiwemo mkakati wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa watu na uhifadhi wa mazingira pamoja na mpango wa kuinua Mkoa wa Kigoma (The Kigoma Joint Programme) unaofadhiliwa na Umoja huo kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 55 ambao ni mradi wa miaka minne unaotekelezwa kuanzia mwezi wa Septemba mwaka huu.
Sherehe ya kuadhimisha miaka 72 ya umoja wa mataifa hufanyika kila mwaka kwa nchi wananchama na kwa mwaka hapa nchini, sherehe hiyo itafanyika katika ukumbi wa karimjee na itakuwa na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda na utunzaji mazingira kwa maendeleo endelevu.”
Sherehe hiyo itahudhuriwa na zaidi ya wageni 500 kutoka hapa nchini na nje ya nchi wakiwemo watumishi wa serikali, watumishi wa sekta binafsi, mabalozi wa mataifa mbalimbali wanaowakilisha nchi zao, vijana pamoja na wanafunzi kutoka katika shule vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya juu.