[caption id="attachment_35144" align="aligncenter" width="900"] Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface akimtakia kila la kheri Dkt Hamisi Kigwangalla baada ya kuruhusiwa kutoka wodini.[/caption] [caption id="attachment_35145" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface,Kulia ni Mkuu wa wodi aliyolazwa Dkt Kigwangalla SR Happyness Mligo.[/caption]
Na; Mwandishi Wetu- MOI
Jopo la Madaktari Bingwa wa MOI linalomhudumia Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla limemruhusu kutoka wodini baada ya kujiridhisha kwamba afya yake imetengamaa na anaweza kurejea nyumbani ili kuja hospitali kama mgonjwa wa nje.
Jopo hilo la madaktari bingwa 5 wa kada za Mifupa, Usingizi na magonjwa ya ndani limefikia maamuzi hayo baada ya kumhudumia Dkt. Kigwangalla toka tarehe 12/08/2018 alipohamishiwa katika taasisi ya tiba ya Mifupa MOI kwaajili ya matibabu ya kibingwa ya mkono wake wa kushoto baada ya kupata matibabu mengine katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt.Respicious Boniface amemtakia kila kheri Dkt Kigwangalla katika kutekeleza majukumu yake ya kitaifa kwani ni muda muafaka wa kwenda kuwatumikia wananchi.
“Kwaniaba ya jumuiya ya Taasisi ya Mifupa MOI, tunakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako ya ujenzi wa Taifa, ilikuwa heshima kubwa kuwa nawe hapa kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja, tunaamini umeridhishwa na huduma zetu na kama kuna mahali umeona mapungufu ni vyema ukatujulisha ili turekebishe” Alisema Dkt Boniface.
Dkt. Boniface amemueleza Dkt. Kigwangalla kwamba kwa kuwa yeye ni daktari itakua rahisi kubaini mabadiliko yoyote ambayo sio ya kawaida na hivyo kushauriana na madaktari wa MOI ili kupata ufumbuzi.
Kwa upande wake Dkt. Kigwangalla ameushukuru uongozi wa Taasisi ya MOI ,madaktari na wauguzi ambao wamekuwa wakimhudumia katika kipindi chote alipokuwa wodini
“Nichukue fursa hii ya kipekee kuwashukuru watoa huduma, watanzania wote ambao mmekua mkiniombea na kunitembelea hapa hospitali baada ya kupata ajali, namshukuru Mungu afya yangu inaendelea vizuri sasa na nimeruhusiwa kwenda nyumbani” alisema Dkt Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari tarehe 4/08/2018 na kupata matibabu ya awali mkoni Manyara kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili na baadae katika Taasisi ya Mifupa MOI.