[caption id="attachment_20359" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa nne kushoto), Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Nne kulia) wakiwa katika Ofisi ya Waziri wa Nishati jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Dkt. Salim Al Ismaily (wa tatu kulia), Naibu Waziri wa Utalii wa Oman, Maitha Al Mahrouqi, (wa pili kulia), Balozi Mteule wa Oman hapa nchini, Ali Al Mahruqi (wa kwanza kulia). Wengine ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa tatu kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kushoto), na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Abdallah Kilima, (wa kwanza kushoto).[/caption]
Na: Teresia Mhagama, DSM
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi wamekutana jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano lengo likiwa ni kuendeleza Sekta ya Nishati nchini.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam ambapo Waziri huyo kutoka Oman aliambatana na Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Naibu Waziri wa Utalii na Balozi wa Oman nchini Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania, viongozi mbalimbali walishiriki katika majadiliano hayo akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Katibu Mkuu, Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo na watendaji wengine kutoka Idara ya Nishati na Sheria.
[caption id="attachment_20362" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kulia), Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Dkt. Salim Al Ismaily (wa tatu kushoto), Naibu Waziri wa Utalii wa Oman, Maitha Al Mahrouqi, (wa pili kushoto), Balozi Mteule wa Oman hapa nchini, Ali Al Mahruqi (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa nne kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa Tatu kulia), Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Abdallah Kilima, (wa pili kulia).[/caption]Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Rumhi, alisema kuwa lengo la Ujumbe huo kufika wizarani ni kujadiliana na watendaji wa Wizara ya Nishati kuhusu maeneo ambayo ingependa ishirikiane na nchi hiyo ya Oman na kwamba nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania.
“ Hapo zamani, Sisi Oman hatukutumia Gesi yetu vizuri kwa kuwa tulifanya haraka kuiuza nje ya nchi lakini ninyi mnayo fursa sasa ya kuitumia gesi yenu ndani ya nchi ili kutengeneza ajira pamoja na kuiendeleza kwa matumizi mbalimbali, na ikiwa ziko fursa za ushirikiano ili kuendeleza nishati hii, sisi tupo tayari,” alisema Dkt. Rumhi.
Akizungumzia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Oman, Dkt. Rumhi alisema kuwa, nchi hiyo inauthamini undugu uliopo na kwamba watalizingatia hilo katika kutekeleza miradi ya ushirikiano ambayo itahusisha wasomi watanzania ambao wameonyesha kuwa na uwezo wa kuendeleza Sekta ya Nishati.
[caption id="attachment_20363" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kulia), Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Tatu kushoto) wakiagana mara baada ya kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Dkt. Salim Al Ismaily (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Utalii wa Oman, Maitha Al Mahrouqi, (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa nne kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa Tatu kulia), Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Abdallah Kilima, (wa pili kulia).[/caption]Kwa upande wake Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt Kalemani, alisema kuwa Tanzania imegundua Gesi Asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.25 huku matumizi yakiwa ni chini ya asilimia 30 hivyo bado kuna Gesi ya kutosha kwa ajili ya miradi mipya ya uzalishaji Umeme na katika kuanzisha viwanda kama vya kemikali na mbolea.
Alisema kuwa kwa sasa Umeme unaotumika nchini, unazalishwa kwa kutumia Gesi Asilia kwa zaidi ya asilimia 50 na kueleza kuwa, Serikali inahitaji kuzalisha Umeme mwingi zaidi kwa kutumia Gesi hiyo.
“ Pamoja na hayo kwa leo napenda kuomba mambo manne ya ushirikiano ambayo yatawafaidisha watanzania. Jambo la kwanza ni kuendeleza ushirikiano katika utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika na Bonde la Eyasi Wembere ambayo katika tafiti za awali yameonesha kuwa na viashiria vya mafuta, hivyo ni muhimu kushirikiana katika tafiti zinazofuta na hatimaye kuthibitisha endapo maeneo hayo yana mafuta kama viashiria vinavyoonesha,” alisema Dkt Kalemani.
Alitaja eneo la Pili ambalo Tanzania inahitaji ushirikiano ni kujenga uwezo wa Wataalam ikiwemo utoaji wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa kuwa Tanzania bado inakua katika Sekta ya mafuta na Gesi hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuwa na wataalam wengi zaidi.
Alitaja jambo la Tatu la ushirikiano kuwa ni uzalishaji Umeme kwa kutumia Gesi asilia jambo litakalopelekea gharama za nishati hiyo kupungua kwa wateja na vilevile kuongeza kiasi cha Umeme nchini tofauti na megawati 1451 zilizopo sasa kwani lengo ni kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
“Jambo la Nne, ni nchi ya Oman kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania katika mradi wa usambazaji Gesi majumbani, viwandani na kwenye magari jambo litakalopelekea ajira kwa wananchi wetu, kutunza mazingira na kuongeza idadi ya viwanda nchini ikiwemo kiwanda mnachotarajia kujenga hapa nchini,” alisema Dkt Kalemani.
Alisema kuwa kwa sasa mradi wa majaribio ya usambazaji Gesi majumbani umeshaanza, ambapo nyumba 70 zimesambaziwa Gesi hiyo jijini Dar es Salaam huku lengo likiwa ni kuendelea kusambaza Gesi hiyo jijini Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na kisha katika mikoa mingine nchini.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alishukuru Ujumbe wa Oman kwa kuitembelea Wizara ya Nishati na Ujumbe huo kutoa matumaini katika kuyafanyia kazi maombi ya Waziri wa Nishati na kwamba ana imani undugu baina ya pande hizo mbili utaendelezwa hasa katika kuendeleza miradi ya Nishati nchini.