Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Kalemani na Mhe. Zungu Wakagua Mabwawa ya Mtera na Kidatu
May 08, 2020
Na Msemaji Mkuu

  • [caption id="attachment_52459" align="aligncenter" width="524"] Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani (wa pili kulia) Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu (wa tatu kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said (wa kwanza kulia) wakiwasili kwenye ukaguzi wa Bwawa la Mtera ambalo lipo Mkoani Iringa.[/caption]

    Hafsa Omar - Morogoro -Iringa

    Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani amefanya ziara ya kikazi kwenye vituo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu vilivyopo mkoani Morogoro na Iringa.

    Katika ziara yake hiyo aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan  Zungu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

    Akizungumza na Waandishi wa Habari, wakati akiwa kwenye ziara hiyo, Dkt. Kalemani alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa maji ya kutosha ya kuzalishia umeme wa kutosha na wa uhakika yanapatikana pamoja na kuangalia athari za mazingira kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

    [caption id="attachment_52460" align="aligncenter" width="720"] Picha ya taswira ya bwawa la Kidatu ambalo Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani na Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu walifanya ziara ya ukaguzi kwenye Bwawa hili lililopo Mkoani Morogoro.[/caption]

    Dkt. Kalemani alisema, kufuatia athari zilizojitokeza kipindi cha mvua wameunda timu ambayo itakuwa chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said itakayoshirikisha wataalam mbalimbali ili kuja na mipango ambayo itasaidia kuondoa athari zilizojitokeza katika mabwawa hayo.

    Amesema kuwa, Bwawa la Kidatu lina kimo cha mita 450 ambacho ndio kimo chake cha juu cha kujaa kwa maji na ikitokea yamejaa zaidi ya hapo yanahitajika kufunguliwa, na kuruhusiwa  kwenda mbele ili kwenda kulijaza bwawa la Rufiji, na kuwataka wataalamu wanaohusika na shughuli hiyo kuhakikisha wanapoyafungulia hayaleti madhara yoyote ya kimazingira.

    Ameongeza kuwa,waatalam hao wanapofungulia  maji hawapaswi kuyafungulia na kuyaacha yakizagaa badala yake wayafungulie ili kwenda kwenye mkondo wake unaostahili, kwa kuwa yanapozagaa ndio madhara yanapotokea  kwa wananchi ambao wanaishi kandokando ya maeneo hayo.

    “ Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha maji hayaleti madhara, nilipokuja kipindi cha nyuma niliona madhara kwenye baadhi ya maeneo na ndio maana nikaunda timu kupitia kwa Katibu Mkuu na baadhi ya viongozi wa mikoa inayozunguka bwawa hili wafanye uratibu ili kuhakikisha yasiendelee kuleta madhara kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo, lazima tuyalinde mazingira yetu” alisema Dkt. Kalemani.

    Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya mito kuwa wachukue tahadhari ili wasije wakaathirika kipindi cha mvua kubwa na kuwataka kutunza vyanzo vya maji na kulima kwa ustaarabu bila kuathiri vyanzo hivyo.

    Pia, amewataka waatalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kipindi ambacho kuna maji ya kutosha na umeme uzalishwe wa kutosha na wahakikishe kuwa umeme hauzimwi nchini kwa sababu hakuna sababu ya kufanya hivyo katika kipindi hiki.

    Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan, amesema lengo la Serikali ni kulinda vyanzo vya maji kwa sababu maji yakikosekana umeme utashindwa kuzalishwa nchini na umeme usipozalishwa uchumi wa nchi yetu utayumba kwani nchi inategemea umeme na umeme wa bei chini ni umeme unaotokana na vyanzo vya maji.

    “vyanzo vya maji vilindwe, vyanzo hivi visipolindwa vitashindwa kusafirisha maji kwenda kwenye miradi mikubwa kama mradi wa umeme wa Julius Nyerere kwa hiyo lazima tulinde vyanzo vyetu kwa umakini zaidi”, Alisema.

    Aidha, amesema ametoa siku kumi kwa timu iliyoundwa ambayo ipi chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutoa taarifa rasmi ya namna gani sasa ya kwenda kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na umeme wa uhakika unapatikana nchini.

    Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, amesema kuwa yeye na pamoja na timu ambayo imeundwa watakaa na wataalam mbalimbali ili kuangalia data za miaka ya nyuma ili waweze kuona watazitumiaje kuweka mipango ya kuzuia uharibifu usitoke kwenye vyanzo hivyo vya umeme.

    •  
    •  
                 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi