Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt . Kalemani atoa mwezi mmoja kwa Vijiji vya Arusha kupata umeme.
Sep 07, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Zuena Msuya, Arusha.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa mwezi mmoja kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyopo katika Jiji la wa Arusha vinaunganishwa na huduma ya umeme.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo jijini Arusha  baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA III) katika Vijiji vilivyopo jijini humo  na kujionea hali ya ukosefu wa nishati ya umeme.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, Wananchi hawafurahii kucheleweshewa kupata  huduma ya umeme hali ya kuwa wengine walikwishalipia huduma hiyo.

"Haipendezi na haifurahishi machoni mtu kajitahidi kujibana na kujenga nyumba yake nzuri na ya kisasa, lakini anakosa umeme wakati uwezo wa kumuunganishia upo na vifaa vipo, sasa  kwa nini asiunganishwe?," alihoji Dkt. Kalemani.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka TANESCO kuunda vikosi kazi mbalimbali vitakavyosaidia kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi kwa haraka.

Aidha, alimwagiza mkandarasi anayesambaza umeme jijini humo, kampuni ya Nipo Group, kuhakikisha kuwa anawafungia umeme wananchi wa Kimondorosi katika Kata ya Olasiti  mkoani Arusha na kuhakikisha kuwa  kila siku anatoa ripoti ya utekelezaji wa mradi kwa mtendaji wa mtaa huo  hadi atakapomaliza kuweka umeme kwa wananchi .

Alisema kuwa, mkandarasi huyo anapaswa kufanya kazi hiyo ili kuwaondolea kero ya ukosefu wa umeme wananchi hao ambao wamekaa kwa muda mrefu bila kupata huduma hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kutoa agizo hilo litakalopelekea wananchi hao kupata umeme kwani wananchi hao walishamlalamikia kuhusu kukosa huduma hiyo.

Vilevile, mmoja wa wananchi katika Kata hiyo, Clementina Mushi alimuomba Waziri wa Nishati kuhakikisha kuwa umeme huo unafika kwa wananchi wote bila kurukwa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi