Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Jafo Atoa Siku 45 Kukamilishwa Mradi wa Maji
Dec 24, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa umepewa siku 45 kukamilisha usimikaji wa mabomba na matanki ya kuhifadhi maji safi na salama kwenye Vijiji vya Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea katika Wilaya ya Mpwapwa.

Agizo hilo limetolewa leo Desemba 23, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na unatekelezwa katika Wilaya tano nchini ambazo ni Mpwapwa, Mvomero, Kishapu, Simanjiro na Kaskazini – A

Akiwa wilayani Mpwapwa katika Kijiji cha Nghambi, Dkt. Jafo amekasirishwa na kitendo cha mkandarasi wa Kampuni ya Make  Engineering  kutoka Dar es Salaam kutokamilisha kwa wakati mradi wa uchimbaji wa visima vyenye urefu wa mita 150 na kumuagiza mkandarasi huyo kukamilisha kazi mapema iwezekanavyo.

Amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha huduma zinasogezwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

"Natoa siku 45 tu maji yaanze kutoka hapa, mradi huu ukamilike. wananchi hawa wanataka maji mapema, hakuna kwenda sikukuu na watumishi acheni kukaa maofisini, simamieni hili kikamilifu" Alisisitiza Dkt. Jafo.

Aidha, ametoa rai kwa wakazi wa Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa kupanda miti kwa wingi ili kulinda mazingira, na kusisitiza kuwa agenda ya mazingira ndio kipaumbele cha Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Josephat Maganga amesema atahakikisha ndani ya siku 45 kazi zote zinakamilika na huduma ya maji inatolewa kwa wananchi.

Mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini unafadhiliwa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Nchi Maskini  kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa visima, ujenzi wa josho, uchimbaji wa lambo na utengenezaji wa majiko banifu. Miradi yenye jumla ya Tshs. 2,257,042,400/- imeidhinishwa kutekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi