Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesisitiza jamii kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia na kuacha matumizi ya kuni na mkaa.
Dkt. Jafo ameyasema hayo wakati akiongea na viongozi mbalimbali katika zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma leo Januari 30, 2024.
Amesema matumizi ya nishati mbadala ni nafuu kuliko matumizi ya mkaa na kuni ambayo huaribu mazingira kwa ukataji wa miti ili kupata mkaa na kuni zinazotumika.
“Tunapoelekea Aprili 26, 2024 Watanzania wanapashwa kuenzi siku hiyo kwa kupanda miti ili kutunza mazingira, Ofisi ya Makamu wa Raisi imeona vyema kuenzi Muungano kwa aina ya kupanda miti ili kutunza mazingira sababu hali ya mabadiliko ya tabianchi yamekuwa makubwa.
“Ukienda maeneo mbalimbali hali sio nzuri hivyo tuna kila sababu ya kutunza mazingira yetu na kila mtu apande mti sababu tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi za umma na binafsi zianze mchakato wa kubadili matumizi ya kuni na mkaa.
Ameongeza kuwa shule nyingi zilizokuwa zinatumia kuni na mkaa kwa sasa zinatumia gesi hivyo hata gharama zimepungua kutokana na matumizi ya gesi hivyo kuokoa pesa nyingi ambazo walikuwa wakizitumia kwenye matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema tuendeleze kampeni ya kutunza vyanzo vya maji ili viweze kutimiza lengo lililokusudiwa.
“Tutaendelea kuhamasishana na kuhamasisha wengine na kuelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya nishati mbadala ili kuendelea kutunza mazingira na kuacha kukata miti kwa ajili ya mkaa,” alisema Mhe. Khamisi.
Katika zoezi hilo, jumla ya miti 600 imepandwa kwenye eneo la Mji wa Serikali Mtumba ikiwa ni katika kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanayotarajiwa kufanyika Aprili 26, 2024.