Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Biteko Akutana na Wazee na Viongozi wa Dini Wilayani Bukombe
Dec 31, 2023
Dkt. Biteko Akutana na Wazee na Viongozi wa Dini Wilayani Bukombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali wilayani Bukombe mkoani Geita pamoja na Wazee wa wilaya hiyo katika mkutano uliolenga kubadilishana mawazo na kumshukuru Mungu kwa mwaka 2023.
Na Teresia Mhagama

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali wilayani Bukombe pamoja na Wazee wa wilaya hiyo, katika mkutano uliolenga kubadilishana mawazo na kumshukuru Mungu kwa mwaka 2023.

 

Mkutano huo umefanyika tarehe 31 Desemba 2023, Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Bukombe.

 

“Mimi pamoja na wenzangu serikalini tunawashukuru sana wazee na viongozi wa dini wa Bukombe kwa ushirikiano mkubwa mnaotoa kwetu, leo nimeona tupate nafasi ya kumshukuru Mungu pamoja na ninyi na kubadilisha mawazo kwani hakuna kiongozi anayeweza kufanya jambo lolote bila kushirikishana na wenzake, ninyi mmeona mengi kuliko mimi, mnafahamu mengi, mnajua mengi, uelewa wenu ni mkubwa na pia mnakaa na jamii muda wote hivyo mnafahamu wapi turekebishe ili tutengeneze Bukombe bora zaidi.” Amesema Dkt. Biteko

 

Ili kuwa na jamii iliyo bora, Dkt. Biteko amewaasa viongozi hao wa dini na wazee kuendelea kukemea matendo mabaya pale wanapoyaona, tena bila kuyaonea aibu kwani ni watu wanaoheshimika katika jamii na ujumbe kutoka kwao unawafikia watu wengi.

Pamoja na kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Bukombe ikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Hospitali, usambazaji umeme na barabara, Dkt. Biteko amesema kuwa, changamoto zozote ambazo bado zipo wilayani humo zitatatuliwa ili Bukombe iweze kuwa bora zaidi.

 

Katika mwaka 2024, Dkt. Biteko ametoa ujumbe wa watu wa makundi yote kupendana na kusameheana na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi ili watoto wasome kwenye shule nzuri, wananchi watumie barabara nzuri, wahudumiwe katika zahanati, kituo cha afya na  hospitali nzuri, wapatiwe huduma ya umeme na maji hali itakayofanya pia watu kupenda maeneo walikotoka.

 

Kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, Wazee wa Bukombe walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu maeneo ambayo wanaona kuwa yanahitaji uboreshaji na pia walimpongeza Dkt. Biteko kwa kuwapa nafasi za kuwasikiliza na kutoa ufafanuzi wa hatua mbalimbali ambazo Serikali inachukua ili kuboresha huduma kwa wananchi wilayani Bukombe.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi