Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dira Mpya Kuifanya Tanzania Kinara wa Chakula Duniani
Dec 09, 2023
Dira Mpya Kuifanya Tanzania Kinara wa Chakula Duniani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Lawrence Mafuru pamoja na baadhi ya Watumishi wa Tume hiyo na Wajumbe wa Bodi wakati wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 9 Desemba, 2023.
Na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Dira ya Maendeleo ni andiko maalum linaloainisha mipango iliyowekwa, mikakati itakayotekelezwa na rasilimali zitakazotumika katika kipindi kilichowekwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla.

Amesema hayo leo Desemba 9, 2023 jijini Dodoma wakati akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa Maendeleo ya mwaka 2050

“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2020-2025 ilijengwa juu ya nguzo kuu nne za kuboresha hali ya maisha ya Tanzania, kuwepo kwa mazingira ya amani, utulivu na umoja, kujenga utawala bora na utawala wa sheria na kujenga uchumi imara unaoweza kuhimili ushindani kutoka nchi nyingine”, amesema Mhe. Rais Samia.

Ameongeza kuwa katika  kilimo, Tanzania imefanya vizuri na kuwa sasa inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 na huku ikielekea asilimia 140 ifikapo mwaka 2025.

“Dira mpya itakayoandikwa, itilie maanani kwamba dunia inakabiliwa na uhaba wa kutokuwa na usalama wa chakula. Matarajio ya Dira inayoandikwa ni kuweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha  uzalishaji wa chakula kwa ajili ya Bara la Afrika na kwingineko duniani”, amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Dira  inayotekelezwa sasa ina maeneo makubwa matano ambayo ni hali ya juu ya maisha bora, kulinda amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na yenye ari ya kujifunza na uchumi imara, endelevu na wenye faida kwa wote.

Mhe. Prof. Mkumbo ametolea mfano mafanikio ya Dira hiyo ikiwemo kulinda amani na utulivu na mshikamano wa taifa  na kupunguza watoto wenye udumavu.

“Wakati tunaanza kutekeleza Dira hii ya sasa, mwaka 2000 asilimia 20 pekee waliokuwa wanamaliza darasa la saba ndiyo walikuwa wanaweza kwenda kidato cha kwanza, sasa tumefika asilimia 70 kwa takwimu za 2022. Lengo letu ifikapo 2025 tufikie asilimia 90”, amesema Prof. Mkumbo.

Ameongeza “ Wakati tunaanza Dira mwaka 2000, ni asilimia 32 pekee ya Watanzania waishio vijijini ndiyo walikuwa na upatikanaji wa maji safi na salama na tumejiweka lengo kwamba ifikapo mwaka 2025 tuwe tumefikia asilimia 85, kwa takwimu za 2022 tupo asilimia 77”.

Naye, Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni Dira ya pili kuandikwa nchini ambayo itadumu na kuongoza mustakabali wa maisha ya Watanzania kwa miaka 25 ijayo.

Mchakato wa Dira unatajwa kuwa katika awamu tatu, ushirikishaji wa wadau katika awamu ya pili ambao utafanyika kupitia mkutano mkuu wa pili wa kitaifa ili  kusaidia kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu maudhui ya Dira mpya na zoezi la uelimishaji umma litakuwa endelevu kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi