Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dira 2050: Serikali Yajipanga Kuimarisha Ufuatiliaji wa Mipango ya Maendeleo
Apr 16, 2026
Dira 2050: Serikali Yajipanga Kuimarisha Ufuatiliaji wa Mipango ya Maendeleo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya ofisi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/2027, Aprili 16, 2026, Bungeni, Jijini Dodoma
Na Adelina Johnbosco – MAELEZO, Dodoma.

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango imesema itaongeza nguvu katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha mafanikio ya Dira 2050 kwa manufaa ya wananchi wote.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya ofisi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, bungeni jijini Dodoma.

Prof. Mkumbo amesema Tume hiyo itajikita katika kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27, pamoja na miradi fungamanishi kupitia wizara za kisekta, ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi.

Aidha, amesema Tume itaendelea kubainisha maeneo ya kukuza sekta binafsi na kuratibu programu mbalimbali za kuondoa umaskini nchini.

“Tutaimarisha matumizi ya tafiti, takwimu na ubunifu katika upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, sambamba na kufuatilia vipaumbele vya Taifa na kutathmini rasilimali za nchi,” amesema Prof. Mkumbo.

Katika kuimarisha ushirikishwaji wa sekta binafsi, amesema Serikali itaendelea kufanya majadiliano na midahalo ya kiuchumi ili kufuatilia mwenendo wa uchumi wa kikanda na kimataifa, pamoja na kupendekeza hatua stahiki za usimamizi wa uchumi.

Kwa upande wa vijana, Prof. Mkumbo amesema Serikali itatenga maeneo maalum ya uwekezaji kupitia mpango wa Youth Industrial Special Economic Zones, utakaowezesha vijana kupata ardhi kwa ajili ya kuanzisha viwanda.

Maeneo hayo yatapatikana katika mikoa ya Dodoma (Nala), Singida (Musisiri–Iramba), Pwani (Kwala na Bagamoyo), Mara (Bunda) na Ruvuma (Songea).

Ameongeza kuwa maeneo mengine ya kipaumbele ni pamoja na kuongeza ardhi ya uwekezaji, kuandaa mikakati ya kuvutia uwekezaji wa kimkakati, kuimarisha mauzo ya nje, kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuimarisha uwekezaji wa umma.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo, akibainisha kuwa wananchi wanapaswa kuelewa nafasi yao katika kufanikisha malengo ya Dira 2050.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor