Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DC Chongolo Amtaka Mkandarasi Anayejenga Soko la Tandale Kuongeza Kasi ya Ujenzi
Aug 18, 2020
Na Msemaji Mkuu

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akitoa maelekezo kwa Meneja mradi wa Kampuni ya ujenzi NAMIS CORPORATE L.T.D  Mhandisi James Msumari mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa soko hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya NAMIS CORPORATE L.T.D ambaye anajenga soko la Tandale kuongeza kasi ya ujenzi huo ili Wafanyabiashara waweze kurudi kwenye eneo lao.

Mhe. Chongolo ameyasema hayo alipofanya ziara katika soko la Tandale na kukuta wafanyabiashara wakiwa katika mazingira yasiyo rafiki hali inayopelekea usumbufu wa shughuli zao na kumuelekeza mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kuondokana na adha inayowakabili.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akipata maelezo kutoka kwa Meneja mradi wa Kampuni ya ujenzi NAMIS CORPORATE L.T.D Mhandisi James Msumari namna ambavyo Soko hilo litakavyokuwa.

Amesema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha miundo mbinu yote ya masoko ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara na kuendesha maisha yao na hivyo kuziwezesha Halmashauri kufikia malengo hayo.

Amefafanua kuwa mradi huo wa soko la kisasa unajengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 8.7 fedha ambazo zimetolewa na Serikali kuu na kwamba tayari mkandarasi huyo ameshalipwa fedha zote na hivyo kusisitiza kwamba anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ilikukamilisha kazi yake kwa wakati.

“Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli imemlipa mkandarasi pesa zote, hivyo hatudai badala yake sisi ndio tunamdai soko letu atukabidhi kwa wakati sahihi, wafanyabishara na wananchi wanasubiria kwa shauku kubwa sana ukizingatia soko hili ni muhimu kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwa sababu litahusika zaidi na biashara ya mazao ya nafaka pamoja na bidhaa nyingine”, amesema Chongolo.

Awali Meneja kutoka kampuni hiyo iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa Soko hilo, Mhandisi James Msumari alimueleza Mhe. Chongolo kuwa ujenzi huo utachukua miezi 12 jambo ambalo alionesha kutokuridhishwa na muda huo na kusema kuwa hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kwakuwa fedha wanazo hivyo  wanapaswa kukamilisha ujenzi kwa makubaliano yaliyoingiwa.

Kwa upande wake Mhandisi Msumari amesema wamepokea maagizo na wako tayari kuyatekeleza ili waweze kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa eneo hilo.

Imeandaliwa na

Kitengo cha Habari na Mahusiano

Manispaa ya Kinondoni.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi